• HABARI MPYA

    Monday, November 18, 2013

    SIMBA SC YAANZA NA MOTO MKALI KOMBE LA UHAI, YAIFUMUA OLJORO 3-0 KARUME

    Na Saada Akida, Ilala
    SIMBA SC imeanza vyema michuano ya timu za vijana za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 3-0 JKT Oljoro ya Arusha kwenye Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam jioni hii.
    Shujaa wa Simba SC jioni ya leo, alikuwa ni mshambuliaji Ibrahim Hajibu aliyefunga mabao mawili dakika ya 27 na 42, wakati bao lingine lilifungwa na beki wa kushoto Miraj Athumani dakika ya 48.
    Hajibu alifunga bao la kwanza baada ya kupokea krosi ya Miraj Athumani na kuunganishwa kwa kichwa maridadi nyavuni, wakati la pili alifunga kwa shuti la umbali wa mita 19 baada ya kupokea pasi ya Miraj pia.
    Miraj Athumani akimrukia Ibrahim Hajibu kumpongeza baada ya kufunga leo Uwanja wa Karume

    Miraj yeye alifunga bao lake baada ya kupokea pasi ya Issa Abdallah, kufuatia gonga safi zilizoanzia kwenye eneo lao.
    Pamoja na kufungwa Oljoro walionyesha upinzani kwa Simba SC, tatizo tu ilikuwa ni ukuta imara wa makinda ya Msimbazi ulioongozwa na Hassan Isihaka na kipa Abuu Hashimu, ambao wote pia wanachezea timu ya kwanza ya Simba SC.
    Katika mchezo mwingine wa leo asubuhi, Ashanti United iliifunga 1-0 Ruvu Shooting, bao  pekee la Issa Suleiman dakika ya 59 Uwanja huo huo wa Karume. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abuu Hashimu, Miza Abdallah, Emil Mgeta, Hassan Isihaka, Carlos Potas, Said Ndemla/Sultan Shija, Mohamed Salum/Jesse Nyombo, Abdul Salum, Issa Abdallah, Ibrahim Hajibu, Miraj Athumani.
    JKT Oljoro; Frank Humbo, Seif Said, Ramadhan Mwinyimbegu/Alphonce Emmanuel, Adam Kindemba, Asira Hamisi, Huba Hilal/Sospeter John, Rashid Kalaga, Charles Sunza, Gunda Kumenya, Josephat Semfukwe/Nelson Otaru na Shamir Fakir. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAANZA NA MOTO MKALI KOMBE LA UHAI, YAIFUMUA OLJORO 3-0 KARUME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top