• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 22, 2013

  RAGE AWASILI KISHUJAA, MAMIA WAMLAKI UWANJA NDEGE, ASEMA YEYE BADO MWENYEKITI SIMBA, HANS POPPE NAYE…

  Na Mahmoud Zubeiry, JNIA
  MWENYEKITI wa Simba SC, Ahaj Ismail Aden Rage amewasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam usiku huu akitokea Sudan na kusema kwamba; “Mimi bado Mwenyekiti wa Simba SC,”.
  Rage aliwasili kwa ndege ya shirika la Kenya saa 1:40 usiku na kutokea mlango wa Watu maalum (VIP) ambako alilakiwa na wanachama zaidi ya 200, waliokuwa kwenye mabasi sita aina ya Coaster.
  “Umati huu uliokuja hapa ni kielelezo tosha sana kwamba kiasi gani wanachama wa Simba wana imani na Mwenyekiti wao, sasa leo sitasema mengi, nitakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari kesho saa saba mchana makao makuu ya klabu(Msimbazi),”alisema Rage.
  Rage akiinua mikono juu kishujaa wakati anatoka Uwanja wa Julius Nyerere, Dar es Salaam usiku wa leo

  Alipoulizwa kuhusu kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Jumatatu na kutangaza kumsimamisha, Rage alisema; “Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji haina uwezo wa kumsimamisha Mwenyekiti, usinimalizie utamu Zubeiry, njoo kesho mchana Msimbazi,”alisema. 
  Watu zaidi ya 200 walifika Uwanja wa ndege tangu saa 11 na ushei jioni ya leo kumsubiri Rage wakiimba nyimbo mbalimbali za kumbeza Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na kumpamba Rage huku wakicheza ngoma.
  Na alipowasili walimlaki kwa shangwe na kucheza naye. Ilikuwa bonge la picha na waliofika kumlaki Rage walikuwa watu wa rika na jinsia tofauti, hadi wazee.
  Rage baada ya kuzungumza kwa kifupi na Waandishi wa Habari alisema anaelekea makao makuu ya klabu, ambako wanachama wengine walikuwa huko wanamsubiri. 
  Jumanne wiki hii, Kinesi alisema, Kamati ya Utendaji ilimsimamisha Rage katika kikao chake cha Jumatatu usiku kwa sababu anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).  Alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati. 
  “Rage alisema mkutano usifanyike kwa sababu alikuwa na safari ya nje na kutaka matawi yaendelee kuleta taarifa za katiba, sisi tukaona kikatiba mkutano lazima uendelee kwani alikaidi,”alisema Kinesi.
  Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya ibara ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.
  Hata hivyo, Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, limesema halitambui uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji na kumuandikia barua Kinesi aliyeendesha kikao hicho kumtaka awape muhtasari wa kikao na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.
  Msinipokeel msubirini Rage; Hans Poppe akiwasili JNIA  Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa baraza bado halijajulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini wamekubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.
  “Kwanza mimi na mwenzangu Ramesh Patel (Mjumbe wa Baraza la Wadhamini) tumekubaliana kuna makosa yalifanyika kwenye kikao chao, hivyo uamuzi wao si sahihi. Tulichokifanya tumemuandikia barua Mwenyekiti aliyesimamia hicho kikao, atupe muhtasari wa kilichotokea na pia tufahamu wajumbe waliohudhuria.
  “Sisi hawajatujulisha rasmi, badala yake nasi tumepata taarifa kutokana na vyombo vya habari, na kama unavyojua inawezekana kwenye vyombo vya habari kuna taarifa tofauti na yaliyojitokeza kwenye kikao…
  “Hivyo ndiyo sababu tunataka muhtsari wa kikao ili kwanza tupate uhakika wa mambo, tujue walizungumza nini na masuala kama hayo. Ila kama walijadili kama yanavyoelezwa kwenye magazeti, wamefanya makosa. Katiba haisemi hivyo, ” alisema Kilomoni ambaye amepata kuwa kiongozi wa Simba na pia mchezaji wa timu hiyo.
  Wakati huo huo: Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe naye amewasili leo ndege moja na Rage, ingawa yeye ametokea, Lubumbashi, DRC alipokwenda kwa shughuli zake za kibiashara.
  Hans Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliwavutia wanachama wa Simba SC alipotokea, lakini akawaomba hataki mapokezi, waendelee kumsubiri Rage.
  “Msinipokee tafadhali, nawashukuru, msubirini Rage anakuja huko nyuma, nimemuacha ndani,”alisema. 
  Hans Poppe ni kipenzi cha wapenzi na wanachama wa Simba SC kutokana mchango wake mkubwa anautoa kwenye klabu hiyo wa hali na mali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RAGE AWASILI KISHUJAA, MAMIA WAMLAKI UWANJA NDEGE, ASEMA YEYE BADO MWENYEKITI SIMBA, HANS POPPE NAYE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top