• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 30, 2013

  MALINZI AMUAMBIA RAIS KIKWETE; "NITAHAKIKISHA TUNAANDAA KOMBE LA AFRIKA MWAKA 2019"

  Na Dina Ismail, Dar es Salaam
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amesema kwamba atahakikisha wanakuwa wenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
  Katika hotuba yake wakati wa mapokezi ya Kombe la Dunia lilio katika ziara yake ya siku mbili nchini tangu jana, Malinzi alisema kwamba atafanya hivyo kutekeleza ushauri wa Rais wa Jamhuri ya Muunganpo wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alioutoa mwaka 2009.
  Tutaandaa Fainali za U17 Afrika; Jamal Malinzi ameelezea nia ya uongozi wake kuandaa michuano hiyo 

  “Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28, Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa. Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019,”amesema Malinzi.
  Rais huyo amesema kwamba Fainali hizo uhusisha mataifa nane yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi na timu mbili zinazoongoza makundi hayo, moja kwa moja hujikatia tiketi ya kucheza fainali za dunia za vijana chini ya umri huo.
  “Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine Babayaro na wengine kadhaa. Ili tupate timu nzuri ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019,”alisema.
  Malinzi amesema katika kuboresha kikosi hicho mwaka 2015 watafanya mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa miaka 13, wakati mwaka 2016 watafanya mashindano ya U 14, ambayo mwaka 2017 yatakuwa ya U15 na 2018 yatakuwa ya U16, ambayo anaamini yatawapatia kikosi cha mwisho cha kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.
  “Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020, kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa,”alisema Malinzi.
  “Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Afrika umri chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019,”amesema.
  Malinzi alimuambia Rais Kikwete kwamba kwa mujibu wa kanuni za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika inatakiwa kuonyesha barua ya kuungwa mkono na nchi yake na kwamba wiki ijayo watawasilisha barua hiyo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono na Serikali katika azma hiyo.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALINZI AMUAMBIA RAIS KIKWETE; "NITAHAKIKISHA TUNAANDAA KOMBE LA AFRIKA MWAKA 2019" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top