• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 25, 2013

  YONDAN ASAINI MKATABA MPYA YANGA SC, SASA ‘KUZEEKEA’ JANGWANI

  Na Mahmoud Zubeiry, Gerezani
  KLABU ya Yanga SC imewaongezea Mikataba ya miaka miwili kila mmoja wachezaji wake watano, akiwemo beki wake Kevin Patrick Yondan, ambaye alikuwa ananyemelewa na klabu yake ya zamani, Simba SC.
  Wengine walioongezamikataba ya kuitumikia klabu hiyo ni beki Nadir Haroub 'Cannavaro' hadi 2016, kiungo Athuman Idd 'Chuji' hadi 2016, winga Simon Msuva hadi 2016 na Jerry Tegete hadi 2016 pia. 
  Mwenyekiti wa Kamati ya Maahindano ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.
  "Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.
  Yondan alisaini Mkataba huo juzi mjini Dar es Salaam na sasa atakuwa mali ya Yanga hadi Juni 2016.
  Juni mwakani, Yondan alikuwa anamaliza Mkataba wake wa awali Yanga SC wa miaka miwili na kwa ndoa mpya- maana yake kuna uwezekano mchezaji huyo bora wa Ligi Kuu msimu uliopita atamalizia soka yake Jangwani. 
  Hadi 2016; Yondan amesaini Mkataba Yanga na sasa atadumu Jangwani hadi Juni 2016

  Mambo yanamuendea vizuri Yondan tangu ajiunge na Yanga SC, kwani mbali na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, pia leo ameteuliwa kuwa Nahodha wa kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars. 
  Kocha wa Stars, Kim Pouslen amemtambulisha Yondan kuwa Nahodha mpya wa timu hiyo, anayechukua nafasi ya Juma Kaseja aliyeachwa kwenye kikosi hicho kinachoondoka jioni ya leo kwenda Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Challenge inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.
  Stars imeagwa leo mchana kwa hafla fupi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa bendera na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YONDAN ASAINI MKATABA MPYA YANGA SC, SASA ‘KUZEEKEA’ JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top