• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 25, 2013

  KEVIN YONDAN NAHODHA MPYA STARS, KIKOSI CHAKABIDHIWA BENDERA, KABURU AAHIDI KUREJEA NA KOMBE

  Na Mahmoud Zubeiry, Gerezani
  KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Pouslen amemtambulisha beki Kevin Yondan kuwa Nahodha mpya wa timu hiyo, anayechukua nafasi ya Juma Kaseja aliyeachwa kwenye kikosi hicho kinachoondoka jioni ya leo kwenda Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Challenge inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.
  Katibu wa BMT, Henry Lihaya kushoto akimkabidhi bendera ya taifa, Nahodha wa Kilimanjaro Stars, Kevin Yondan. Kulia ni kocha Kim Poulsen. Chini Yondan anazungumza na Waandishi wa Habari.


  Stars imeagwa leo mchana kwa hafla fupi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa bendera na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya. 
  Kocha wa Stars, Mdenmark Poulsen amesema kwamba anakwenda Kenya kwa lengo moja kubwa kupigana kukata tiketi ya kucheza Robo Fainali kutoka kwenye Kundi lao B, na baada ya hapo mapambano mengine yatafuatia.
  Amesema anafurahi wachezaji wake wako tayari sana kwa ajili ya mashindano hayo na wamemuahidi kufanya vizuri.
  Nahodha mpya, Yondan kwa upande wake amesema kwamba amefurahia wadhifa huo na kwa pamoja na wachezaji wenzake, wanaahidi kwenda kupigana kurejesha heshima ya timu yao iliyopotea kwa sasa.
  Tutarudi na Kombe; Mkuu wa Msafara, Geoffrey Nyange Kaburu katikati akizungumza. Chini kocha Poulsen anazungumza

  “Tunaahidi kwenda kupigana na Mungu atatujaalia tutarudi na Kombe na kurudisha heshima yetu, kwa sababu timu yetu kwa sasa  ni kama imeshuka hivi na kupoteza heshima yake mbele ya wananchi, ila tukirudi na Kombe hapa, heshima itarudi,”alisema.
  Mkuu wa Msafara, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema wanakwenda Nairobi, Kenya kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha Kombe la Challenge linakuja Dar es Salaam.
  Msafara wa Stars iliyotwaa Kombe la Challenge mara tatu, 1974, 1994 na 2010, utaondoka saa 10:00 jioni kwa ndege ya RwandAir.
  Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
  Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
  Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
  Wachezaji wa Stars wakisikiliza hotuba

  Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).
  Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KEVIN YONDAN NAHODHA MPYA STARS, KIKOSI CHAKABIDHIWA BENDERA, KABURU AAHIDI KUREJEA NA KOMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top