• HABARI MPYA

    Thursday, November 21, 2013

    KILOMONI AMBEBA RAGE MAPINDUZI SIMBA

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    SIKU moja baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kudai imemsimamisha Mwenyekiti wake, Ismail Rage, Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, limesema halitambui uamuzi huo.
    Kutokana na hali hiyo, baraza hilo limemuandikia barua Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ aliyeendesha kikao kilichodaiwa kumsimamisha Rage awape muhtasari wa kikao hicho na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.
    Mapinduzi batili; Mzee Kilomoni amesema Rage bado Mwenyekiti halali Simba SC

    Akizungumza na gazeti la Habari Leo jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa baraza bado halijajulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini wamekubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.
    “Kwanza mimi na mwenzangu Ramesh Patel (Mjumbe wa Baraza la Wadhamini) tumekubaliana kuna makosa yalifanyika kwenye kikao chao, hivyo uamuzi wao si sahihi. Tulichokifanya tumemuandikia barua Mwenyekiti aliyesimamia hicho kikao, atupe muhtasari wa kilichotokea na pia tufahamu wajumbe waliohudhuria.
    “Sisi hawajatujulisha rasmi, badala yake nasi tumepata taarifa kutokana na vyombo vya habari, na kama unavyojua inawezekana kwenye vyombo vya habari kuna taarifa tofauti na yaliyojitokeza kwenye kikao…
    “Hivyo ndiyo sababu tunataka muhtsari wa kikao ili kwanza tupate uhakika wa mambo, tujue walizungumza nini na masuala kama hayo. Ila kama walijadili kama yanavyoelezwa kwenye magazeti, wamefanya makosa. Katiba haisemi hivyo, ” alisema Kilomoni ambaye amepata kuwa kiongozi wa Simba na pia mchezaji wa timu hiyo.
    Wakati huo huo, kiongozi wa zamani wa Simba, ambaye hata hivyo alikataa jina lake kuandikwa gazetini aliponda uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba na kusema kuwa viongozi hao walikiuka Katiba ya Simba.
    “Mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba ipo kwenye Ibara ya 30 ya Katiba yetu, inaeleza kazi mbalimbali za Kamati ya Utendaji. Ukienda mpaka Ibara ya 30(m) inasema hata hizo kazi zake kwamba kutoa adhabu ipo, lakini unatoa adhabu kwa nani? Haisemi ipo kimya.
    “Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba inasema kutakuwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti waliochaguliwa na Mkutano Mkuu. Nafasi ya Kaimu Mwenyekiti haipo, kwani inasema ikitokea nafasi yoyote ya uongozi ipo wazi inatakiwa ijazwe ndani ya siku 90. Hakuna Kaimu Makamu Mwenyekiti Simba.
    “Ibara ya 33 inazungumzia majukumu ya Mwenyekiti wa Simba, kwamba ni kuitisha Mkutano Mkuu na Kamati ya Utendaji, sasa kikao chao cha Jumatatu kiliitishwa na nani kama Mwenyekiti alisafiri? Inawezekana Mwenyekiti (Rage) alimwambia waendelee na kikao kwa maana ya vikao vingine lakini si Kamati ya Utendaji,” alisema kiongozi huyo.
    Pia alisema hata kama Katiba ya Simba ingekuwa inaruhusu, lakini uamuzi wa kumsimamisha bila kumpa nafasi ya kujieleza sahihi ni kumnyima haki yake ya msingi.
    “Unamtuhumu mtu, je umewahi kumuita? Ulimpa tuhuma zake ajibu? Kimtazamo wa kisheria huo ni upungufu mkubwa, warudi tena wajipange,” alisema kiongozi huyo.
    Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kinesi alisema, kamati yake iliamua kumsimamisha Rage kwasababu anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).
    Alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati. 
    “Rage alisema mkutano usifanyike kwasababu alikuwa na safari ya nje na kutaka matawi yaendelee kuleta taarifa za katiba, sisi tukaona kikatiba mkutano lazima uendelee kwani alikaidi,”alisema Kinesi.
    Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya ibara ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILOMONI AMBEBA RAGE MAPINDUZI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top