• HABARI MPYA

    Monday, November 25, 2013

    STARS WATUA SALAMA NAIROBI

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    BAADA ya safari ya takriban saa nne angani, hatimaye timu ya soka ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars imeatua salama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Kenya tayari kuwania taji la nne la Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Katika michuano hiyo inayoanza kutimua vumbi Novemba keshokutwa, Stars imepangwa Kundi B pamoja na Zambia, Burundi na Somalia na itafungua dimba na Chipolopolo Alhamisi Uwanja wa Machakos.
    Wachezaji wa Kili Stars wakishuka kwenye ndege Uwanja wa Jomo Kenyatta usiku huu

    Stars imetua hapa saa 2:45 usiku baada ya safari ndefu kidogo wakipitia Kigali, Rwanda kabla ya kutua Nairobi na iliwachukua saa nzima hadi kupanda basi kuelekea hotelini baada ya kukamilisha taratibu za kuingia nchini hapa za Idara ya Uhamiaji.
    Stars iliagwa leo mchana kwa hafla fupi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa bendera na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya. 
    Katika hafla hiyo, kocha wa Stars, Mdenmark Poulsen pamoja na kumtaja beki Kevin Yondan kuwa Nahodha mpya, pia amesema kwamba lengo moja kubwa kupigana kukata tiketi ya kucheza Robo Fainali kutoka kwenye Kundi lao B, na baada ya hapo mapambano mengine yatafuatia.
    Kocha Kim Poulsen akiwa ameuchapa usingizi kwenye ndege na wanaofuatia chini ni Nahodha Kevin Yondan, Ismail Gambo, Ivo Mapunda, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar na Said Mourad, Frank Domayo, Himid Mao, Aishi Manula na Joseph Kimwaga,Hassan Dilunga hajalala na Michael Pius. 












    Amesema anafurahi wachezaji wake wako tayari sana kwa ajili ya mashindano hayo na wamemuahidi kufanya vizuri.

    Nahodha mpya, Yondan kwa upande wake alisema kwamba amefurahia wadhifa huo na kwa pamoja na wachezaji wenzake, wanaahidi kwenda kupigana kurejesha heshima ya timu yao iliyopotea kwa sasa.
    “Tunaahidi kwenda kupigana na Mungu atatujaalia tutarudi na Kombe na kurudisha heshima yetu, kwa sababu timu yetu kwa sasa  ni kama imeshuka hivi na kupoteza heshima yake mbele ya wananchi, ila tukirudi na Kombe hapa, heshima itarudi,”alisema.
    Mkuu wa Msafara wa Stars iliyotwaa Kombe la Challenge mara tatu, 1974, 1994 na 2010, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wanakwenda Nairobi, Kenya kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha Kombe la Challenge linakuja Dar es Salaam.
    Wachezaji walitua na Stars hapa ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
    Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam) na washambuliaji Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Mrisho Ngasa (Yanga).
    Bin Zubeiry na Juma Luizio kushoto

    Kutoka kulia Deo Munishi, Mrisho Ngassa na Bin Zubeiry

    Washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba 1 mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS WATUA SALAMA NAIROBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top