• HABARI MPYA

    Wednesday, November 27, 2013

    RAGE SASA ANATAKA KUHARIBU KABISAAA

    WIKI iliyopita uliibuka mgogoro kama mzaha ndani ya klabu ya Simba SC, kufuatia Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutangaza kumsimamisha Mwenyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage kwa madai anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).
    Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati. 

    Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.
    Hata hivyo, baadaye Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, likasema halitambui uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji na kumuandikia barua Kinesi aliyeendesha kikao hicho kumtaka awape muhtasari wa kikao na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.
    Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa Baraza lake halikujulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini walikubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.
    “Kwanza mimi na mwenzangu Ramesh Patel (Mjumbe wa Baraza la Wadhamini) tumekubaliana kuna makosa yalifanyika kwenye kikao chao, hivyo uamuzi wao si sahihi. Tulichokifanya tumemuandikia barua Mwenyekiti aliyesimamia hicho kikao, atupe muhtasari wa kilichotokea na pia tufahamu wajumbe waliohudhuria.
    “Sisi hawajatujulisha rasmi, badala yake nasi tumepata taarifa kutokana na vyombo vya habari, na kama unavyojua inawezekana kwenye vyombo vya habari kuna taarifa tofauti na yaliyojitokeza kwenye kikao…
    “Hivyo ndiyo sababu tunataka muhtsari wa kikao ili kwanza tupate uhakika wa mambo, tujue walizungumza nini na masuala kama hayo. Ila kama walijadili kama yanavyoelezwa kwenye magazeti, wamefanya makosa. Katiba haisemi hivyo, ” alisema Kilomoni ambaye amepata kuwa kiongozi wa Simba na pia mchezaji wa timu hiyo.
    Katika siku ambayo kikao hicho kinafanyika Jumatatu ya wiki iliyopita, Rage naye alikuwa anasafiri kwenda Sudan kwa shughuli zake za kisiasa.
    Lakini siku moja kabla ya kusimamishwa, Rage alisainisha wachezaji wawili wapya nyumbani kwake Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na fedha ambazo zilitumika kusajili wachezaji hao, inasemekana walichanga nusu kwa nusu, yeye na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe.
    Mapema nilisema huwezi kuona mantiki ya kikao kufanyika bila Rage wakati alikuwepo hadi siku moja kabla ya kikao- na matokeo yake sasa si Baraza la Wadhamini tu, bali hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limeendelea kumtambua mwanasiasa huyo kama kiongozi mkuu wa klabu hiyo.
    TFF imemtaka Rage aitishe Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14, baada ya kubaini kuna mgogoro katika klabu kufuatia kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.
    Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”
    Na TFF imesema itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.
    Hata hivyo, Rage amekataa kuitisha Mkutano akidai atakuwa anakiuka Katiba ya Simba SC. Kimsingi Rage amefanikiwa kushinda jaribio la kumpindua na sasa anaonekana kama kutaka kulipa kisasi kwa wapinzani wake.
    Kweli, Kinesi na kundi lake hawakumtendea haki Rage, lakini sioni kama ni busara kwake kulipa kisasi bila kuzingatia ataiathiri vipi klabu. Rage ni mchezaji wa zamani wa Simba SC (miaka ya 1970) na amekuwa kiongozi wa klabu hiyo kwa mara ya kwanza miaka ya 1980.
    Ajaribu kutazama historia yake na Simba SC halafu ajilinganishe na watu anaopambana nao ni kisha atagundua kwamba anataka kufanya makosa makubwa. Tena sana. Rage ni mkubwa sana katika Simba SC historia yake hakuna hata anayemkaribia kati ya Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji. Anapaswa kutambua hilo.
    TFF imemuagiza kwa nia nzuri tu kuitisha Mkutano Mkuu kusikiliza na kujibu hoja za wanachama kwa sababu hiyo ndiyo njia ambayo inaweza kurejesha amani kwa sasa. Tazama sasa, wenzake wameshazungumza na kocha mpya aje kufundisha timu, lakini yeye anasema makocha waliofukuzwa Alhaj mwenzake Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ bado makocha halali na hamtambui huyo mpya.
    Haya ni matatizo makubwa ambayo yanaletwa Simba SC na kiini chake ni kikao batili cha akina Kinesi. Lakini bado Rage hapaswi kulipa kisasi, kwa sababu hatamuumiza Kinesi wala Ibrahim Masoud ‘Mestro’, bali kipenzi chake mwenyewe, Simba SC. Sasa kwa nini afanye hivyo?
    Vyema Rage akaitisha Mkutano, asikilize hoja za wanachama kwa maslahi ya klabu, maana sasa hamkani si shwari tena pale. Jumatano njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAGE SASA ANATAKA KUHARIBU KABISAAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top