• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 24, 2013

  MZEE KINESI NA WENZAKE WALIVYOMPA ‘USHINDI WA MEZANI’ RAGE…

  JUMANNE wiki hii Kamati ya Utendaji ya Simba SC ilitangaza kumsimamisha Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage katika kikao chake cha Jumatatu usiku kwa sababu anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).
  Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati. 

  “Rage alisema mkutano usifanyike kwa sababu alikuwa na safari ya nje na kutaka matawi yaendelee kuleta taarifa za katiba, sisi tukaona kikatiba mkutano lazima uendelee kwani alikaidi,”alisema Kinesi.
  Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya ibara ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.
  Hata hivyo, baadaye Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, likasema halitambui uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji na kumuandikia barua Kinesi aliyeendesha kikao hicho kumtaka awape muhtasari wa kikao na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.
  Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa Baraza lake bado halijajulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini wamekubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.
  “Kwanza mimi na mwenzangu Ramesh Patel (Mjumbe wa Baraza la Wadhamini) tumekubaliana kuna makosa yalifanyika kwenye kikao chao, hivyo uamuzi wao si sahihi. Tulichokifanya tumemuandikia barua Mwenyekiti aliyesimamia hicho kikao, atupe muhtasari wa kilichotokea na pia tufahamu wajumbe waliohudhuria.
  “Sisi hawajatujulisha rasmi, badala yake nasi tumepata taarifa kutokana na vyombo vya habari, na kama unavyojua inawezekana kwenye vyombo vya habari kuna taarifa tofauti na yaliyojitokeza kwenye kikao…
  “Hivyo ndiyo sababu tunataka muhtsari wa kikao ili kwanza tupate uhakika wa mambo, tujue walizungumza nini na masuala kama hayo. Ila kama walijadili kama yanavyoelezwa kwenye magazeti, wamefanya makosa. Katiba haisemi hivyo, ” alisema Kilomoni ambaye amepata kuwa kiongozi wa Simba na pia mchezaji wa timu hiyo.
  Katika siku ambayo kikao hicho kinafanyika Jumatatu, Rage naye alikuwa anasafiri kwenda Sudan kwa shughuli zake za kisiasa, si inafahamika huyu ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM)?
  Lakini Jumapili Rage alisainisha wachezaji wawili wapya nyumbani kwake Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na fedha ambazo zilitumika kusajili wachezaji, inasemekana walichanga nusu kwa nusu, yeye na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe.
  Mapema nilisema huwezi kuona mantiki ya kikao kufanyika bila Rage wakati alikuwepo hadi siku moja kabla ya kikao- na matokeo yake sasa si Baraza la Wadhamini tu, bali hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limeendelea kumtambua mwanasiasa huyo kama kiongozi mkuu wa klabu hiyo.
  TFF imemtaka Rage aitishe Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia jana, baada ya kubaini kuna mgogoro katika klabu kufuatia kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.
  Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”
  Na TFF imesema itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.
  Sitaki kuzizungumzia tuhuma za Rage kwa sasa kama zina uzito au la, labda siku zijazo nitafanya hivyo- lakini tu si vibaya kuelezea athari moja kubwa ya kikao batili cha Kamati ya Utendaji ni kuvuruga uhusiano baina ya Wajumbe na Mwenyekiti wao bila sababu.
  Jana Rage, alitokea Uwanja wa Karume ambako Simba B ilikuwa inamenyana na Ruvu Shooting katika Kombe la Uhai na Mzee Kinesi alipomuona Mwenyekiti wake huyo akatoa gari lake kwa kasi kukimbia. Yote ya nini haya sasa?
  Kama Wajumbe waliona hawammudu Rage, kwa nini kesi yake wasiipeleke ngazi za juu kwa mfano Baraza la Wadhamini na TFF? Ndiyo, baraza la Wadhamini linaundwa na Kamati ya Utendaji, lakini baada ya hapo linakuwa na mamlaka ya kumulika na kulinda mali za klabu, hivyo unaweza kuona kabisa linao uwezo wa kumrudi Rage au yeyote kutoka Kamati ya Utendaji.
  Lakini badala yake akina Kinesi wakaitisha kikao cha woga woga na kutangaza kumpindua Rage, walichemka sana. Hii wiki yote waliyogombana mambo mangapi ya klabu yamesimama? Na kwa ujumla ugomvi huu usio na kichwa wala miguu umeiathiri kiasi gani klabu?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MZEE KINESI NA WENZAKE WALIVYOMPA ‘USHINDI WA MEZANI’ RAGE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top