• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 27, 2013

  ‘WORLD CUP’ YA AFRIKA MASHARIKI NA KATI YAANZA KUTIMUA VUMBI LEO NAIROBI

  Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
  MICHUANO ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Cup, inatarajiwa kuanza leo mjini Nairobi, Kenya hadi Desemba 12, ikishirikisha timu 12.
  CECAFA ni Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati na lina wanachama 12, na katika kuongeza nakshi katika mashindano yake limekuwa likialika nchi ambazo si wanachama na mwaka huu inmekuja Zambia kuongeza ushindani.
  Kundi A lina timu za wenyeji Kenya,Ethiopia, Zanzibar na Sudan Kusini, Kundi B kuna Tanzania Bara, Zambia, Burundi na Somalia wakati Kundi C kuna mabingwa watetezi, Uganda, Rwanda Sudan na Eritrea.   
  Kombe la Dunia la Afrika Mashariki na Kati: Tanzania Bara wakishangilia taji lao la mwisho la Challenge kutwaa mwaka 2010 mjini Dar es Salaam

  ORODHA YA MABINGWA;

  1973 Uganda      
  1974 Tanzania    
  1975 Kenya       
  1976         Uganda      
  1977 Uganda      
  1978 Malawi      
  1979 Malawi      
  1980 Sudan       
  1981 Kenya       
  1982 Kenya       
  1983 Kenya       
  1984 Zambia      
  1985 Zimbabwe 1986               Haikufanyika
  1987 Ethiopia    
  1988 Malawi      
  1989 Uganda      
  1990 Uganda      
  1991 Zambia      
  1992 Uganda      
  1993         Haikufanyika 
  1994 Tanzania    
  1995 Zanzibar    
  1996 Uganda      
  1997         Haikufanyika 
  1998         Haikufanyika 
  1999 Rwanda B 
  2000 Uganda      
  2001 Ethiopia    
  2002 Kenya       
  2003 Uganda      
  2004 Ethiopia    
  2005 Ethiopia    
  2006 Zambia      
  2007 Sudan       
  2009 Uganda      
  2009 Uganda      
  2010         Tanzania
  2011         Uganda
  2012         Uganda
  Mdhamini Mkuu wa Challenge ya mwaka huu ni Serikali ya Kenya ambayo imetoa dola za Kimarekani 125,000 (zaidi ya Sh. Milioni 140) na kuahidi kutoa zaidi, hivi sasa ikiwa katika mchakato wa kukusanya fedha zaidi.
  Tayari kuna dola za Kimarekani 600,000 (zaidi ya Sh. Milioni 900) zinazotokana na mauzo ya haki za matangazo ya Televisheni yatakayohusu mechi zote 27 za mashindano hayo.
  Gavana wa Machakos, Alfred Mutua naye ametoa Sh. Milioni 5 za Kenya zaidi ya Sh. Milioni 11 za Tanzania kudhamini mashindano hayo, wakati wenzake kutoka Nairobi na Kisumu wametoa Sh Milioni 10 za Kenya, zaidi ya Sh. Milioni 22 za Tanzania.
  Kampuni ya Coca Cola pia imetoa Sh Milioni 6.5 za Kenya (Milioni 5 taslimu na vinywaji vyenye thamani ya Sh. Milioni 1.5), wakati kampuni ya Bima ya UAP itatoa Sh Milioni 5.5 za Kenya (Milioni 2.5 fedha taslimu nan a Milioni 3 kwa ajili ya bima za wachezaji na marefa wote) katika mashindano hayo.
  Kama ilivyothibitishwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Kenya, Sam Nyamweya, Serikali ya Kenya pia inakusanya fedha zaidi za kuongeza kwenye mashindano hayo na hivi karibuni itawasilisha mchango wake.
  Kati ya fedha hizo, dola 60,000 ni kwa ajili ya zawadi za washindi, bingwa akiondoka na dola za Kimarekani 30,000, mshindi wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.
  Japokuwa ukanda wa CECAFA ndiyo eneo linalojikongoja kwa sasa katika soka ya kimataifa, lakini ukweli ni kwamba, mpira wa miguu barani Afrika, ulianzia ukanda wa Afrika Mashariki.
  Michuano ya kwanza kabisa mikubwa barani Afrika, ilihusisha mataifa manne, Kenya, Uganda, Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na Zanzibar, ikijulikana kwa jina la Kombe la Gossage.
  Michuano hiyo ya Gossage ambayo sasa imekuwa Kombe la Challenge, ilifanyika mara 37 kuanzia mwaka 1926 hadi 1966, ilipobadilishwa jana na kuwa michuano ya wakubwa ya soka kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, ilifanyika mara saba kati ya mwaka 1965 na 1971, ilipozaliwa rasmi CECAFA Challenge.
  Sunday Manara anayeambaa na mpira enzi zake
  Tanganyika ilianza kushiriki michuano hiyo tangu mwaka 1945, wakati Zanzibar ilijitosa miaka minne baadaye, 1949.
  Michuano hiyo ilikuwa ikidhaminiwa na bepari aliyekuwa akimiliki kiwanda cha sabuni, William Gossage, aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1799 na kufariki dunia Aprili 9, mwaka 1877.
  Michuano hiyo mikongwe zaidi barani, imekuwa ikiandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikihusisha timu za taifa za ukanda huo.
  Hadi inafikia tamati michuano ya Gossage, Uganda ilikuwa inaongoza kwa kutwaa taji hilo, mara 22, ikifuatiwa na Kenya iliyotwaa mara 12 na Tanzania mara tano.
  Mwaka 2005, michuano hiyo ilifanyika chini ya udhamini wa bilionea wa Ethiopia mwenye asili ya Saudi Arabia, Sheikh Mohammed Al Amoudi na kupewa jina la Al Amoudi Senior Challenge Cup na baada ya hapo Tusker wakachukua nafasi hadi Mkataba wapo ulipomalizika mwaka jana.
  Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga amesema kwamba wapo katika jitihada za kutafuta wadhamini zaidi wa mashindano hayo. Challenge ni michuano inayofanyika ndani ya wiki mbili, lakini imekuwa na msisimko mkubwa tangu enzi.
  Challenge imetoa wachezaji wakubwa waliocheza Ulaya kama marehemu Majid Musisi wa Uganda, Kalusha Bwalya enzi hizo Zambia haijajitoa CECAFA, Dennis Oliech na wengine kadhaa.    
  Sunday Manara alichezea klabu za Almero ya Uholanzi, Odense ya Denmark, Metz ya Ufaransa, Heracles FC Uholanzi, New York Eagles ya Marekani, St. Veit FC ya Austria na Al-Nasri FC ya Dubai alikomaliza soka yake kuanzia mwaka 1981 hadi 1984.
  Kassim Manara, aliyetokea Yanga pia kama kaka yake, alifikia kucheza hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa na klabu ya Klangefurt ya Austria. Baadaye Kassim alikwenda Italia, ambako aliitwa na klabu moja huko, lakini hakuna aliyefanikiwa kuelewa mwisho wake ni nini huko. Tangu aondoke, Kassim hajawahi kurudi Tanzania na kwa sasa anaishi Antwerp, Ubelgiji.
  Dennis Oliech kushoto ni tunda la Challenge sasa anacheza Ulaya
  Oliech alitoa mchango mkubwa kwa Kenya kutwaa ubingwa wa Challenge mwaka 2002 mjini Mwanza.
  Oliech aliyeingia kuchukua nafasi ya Francis Chinjili, aliifungia Kenya bao la ushindi dakika ya 72 katika fainali ya michuano hiyo Desemba 14, mwaka 2002, Uwanja wa Kirumba, Mwanza. Fainali ilikuwa dhidi ya Tanzania Bara.
  Siku hiyo, nakumbuka Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Kilimanjaro Stars katika dakika ya 28, lakini dakika mbili baadaye Paul Oyuga akaisawazishia Harambee Stars, kabla ya Mecky Mexime kuifungia Tanzania Bara bao lililoelekea kuwa la ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 59.
  Lakini wakati mamia ya mashabiki wa Kili Stars waliokuwa wamefurika kwenye majukwaa ya CCM Kirumba wanashangilia ushindi, mshambuliaji anayezeeka na soka yake kama Rogger Milla wa Cameroon au Madaraka Suleiman wa Tanzania; John Baraza alimtungua Juma Kaseja dakika ya 70 na kuisawazishia Kenya bao.
  Bao hilo liliwachanganya wachezaji wa Stars, akina Kaseja, Mexime, Alphonce Modest, Victor Costa, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Ulimboka Mwakigwe, Salvatory Edward, Athumani Machuppa, Emmanuel Gabriel aliyempisha  Zubery Katwila dakika ya 74 na Abdul Mtiro aliyempisha Joseph Mwanakusha dakika ya 69, hivyo kuipa nafasi Kenya kuuteka mchezo.
  Hatimaye Oliech wakati huo aliyekuwa anaichezea Harambee Stars akitokea klabu ya Mathare United ya nyumbani kwao, akamtungua Kaseja na kuzima kabisa matumaini ya Watanzania kushangilia taji la tatu la Challenge.
  Nakumbuka kikosi cha Harambee siku hiyo kilikuwa; Victor Onyango, Adam Shaban, Daniel Agina, George Waweru, Phillip Opiyo, Robert Mambo, Anthony Mathenge, Edward Karanja, Titus Mulama aliyempisha Geoffrey Mangenge ‘Osama’, Francis Chinjili aliyemuachia Oliech, Paul Oyuga aliyempisha Baraza.
  Oliech ndiye alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake matano na hata huo ukawa mwanzo wa safari yake ya Ulaya.
  Baada ya kung’ara kwenye michuano hiyo alichukuliwa na Al Arabi ya Qatar aliyoichezea kuanzia 2003 hadi 2005 kabla ya kuhamia Nantes ya Ufaransa, ambayo ilimuuza Auxerre ambako alicheza hadi mwaka huu alipohamia Ajaccio ya huko huko.
  Na huu si mwisho- kwa jinsi ambavyo soka ya ukanda huu inakuwa kwa kasi siku za karibuni, tarajia kutoka Challenge watapatikana wakali wengine wa kucheza Ulaya. Karibu Challenge cup, ‘World Cup’ ya Afrika Mashariki na Kati.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘WORLD CUP’ YA AFRIKA MASHARIKI NA KATI YAANZA KUTIMUA VUMBI LEO NAIROBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top