• HABARI MPYA

    Thursday, November 28, 2013

    TENGA AIACHA CHALLENGE KWA UCHUNGU NA HASIRA ZAKE SASA…

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    RAIS wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga ameondoka jana mjini hapa kurejea Dar es Salaam kuwahi ziara ya Kombe la Dunia la FIFA, lakini hajaridhishwa kabisa na hali halisi aliyoiacha katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge na amesema ana kazi kubwa ya kufanya kuweka mambo sawa.
    Akizungumza BIN ZUBEIRY jana usiku wakati akijiandaa kwa safari, Tenga alisema kwamba wanakabiliwa na tatizo la fedha za kuendesha mashindano, hali ambayo imefanya mashindano ya mwaka huu yafadhiliwe na Serikali ya Kenya.
    Rais wa CECAFA, Tenga tayari k safari ya kurejea nyumbani Dar es Salaam kuwahi ziara ya Kombe la Dunia na chini akiwa na wadau wa soka Afrika Mashariki na Kati

    Alisema nchini nyingi wanachama wa CECAFA hazina uwezo wa kuandaa mashindano hayo kwa sasa bila msaada wa Baraza hilo na iwapo juhudi za haraka hazitachukuliwa, michuano hiyo iko hatarini.
    Alisema tatizo kubwa anadhani ni wadau na makampuni kupoteza imani na viongozi wa soka wa nchi husika, wakihofia wakitoa fedha zitaliwa.
    “Ilinibidi nisafiri sana kuja Nairobi kuzungumza na makampuni na Serikali ya huku kuwahakikishia wakitoa fedha zitakwenda kutumika katika shughuli husika, nilizungumza hadi na Waziri Mkuu,”alisema Tenga.
    Hata hivyo, Tenga amesema hana imani kwamba kweli viongozi wa nchi za ukanda wake si waaminifu, bali ni imani tu iliyojengeka na akavitaka vyombo vya habari visaidie kuondoa dhana hiyo.
    “Mna jukumu kubwa sana la kutusaidia kuelimisha watu, maana hii pengine inaweza kuwa ni dhana tu, hawa bwana hawaibi fedha, maana hata ukifuatilia huwezi kuona wanaiba wapi, tusaidieni jamani,”alisema Tenga.
    Pamoja na hayo, Tenga amesema ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha CECAFA inakuwa na mdhamini wake maalum wa mashindano hayo ili kuzipunguzia mzigo nchi zitakazopewa uenyeji.
    “Tunataka wao wabaki na jukumu tu la usafiri wa ndani na gharama nyingine ndogo ndogo, lakini mzigo mzima wa mashindano tunaubeba wenyewe. Na nitahakikisha nifanya hivyo ili ndani ya miaka miwili, mambo yabadilike,”alisema Tenga.  
    Michuano ya CECAFA Challenge ilianza jana mjini hapa, Zanzibar ikiifunga 2-1 Sudan Kusini na wenyeji, Kenya wakitoka sare ya bila kufungana na Ethiopia, hizo zikiwa mechi za Kundi A, Uwanja wa Nyayo.
    Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi za Kundi B, Burundi ikimenyana na Somalia na Tanzania Bara wakipepetana na Zambia huko Machakos.
    Mabingwa watetezi, Uganda wao wataanza kampeni za kutetea taji kesho jioni Machakos kwa kumenyana na Rwanda baada ya Sudan na Eritrea kuumana mchana katika mechi za Kundi C.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TENGA AIACHA CHALLENGE KWA UCHUNGU NA HASIRA ZAKE SASA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top