• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 30, 2013

  ZANZIBAR YAPIGWA NA WAHABESHI NYAYO CHALLENGE

  Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
  ZANZIBAR imejiweka njia panda kwenda au kutokwenda Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Ethiopia mchana wa leo, Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
  Mabao yaliyoizamisha Zanzibar leo yalifungwa na Nahodha Fasika Asfan dakika ya tano, Salahadin Bargicho kwa penalti dakika ya 37 baada ya Manaye Fantu kuangushwa kwenye ene la hatari wakati Yonathan Kebede alifunga la tatu dakika ya 83.
  Bao la Zanzibar lilifungwa na kiungo mpya wa Simba SC, Awadh Juma Issa dakika ya 68 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Seif Abdallah Karihe, ambaye alimlamba chenga beki wa kulia wa Ethiopia kwanza.
  Mshambuliaji wa Zanzibar Seif Abdallah Karihe akipasua katikati ya wachezaji wa Ethiopia leo Nyayo

  Zanzibar ilipata pigo mapema tu dakika ya 14, baada ya mchezaji wake tegemeo Suleiman Kassim ‘Selembe’ kuumia nyama za paja na kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Seif Abdallah Karihe.    
  Marefa Louis Hakizimana aliyesaidiwa na Simba Honore wote wa Rwanda na Idam Hamid wa Sudan walionekana wazi kuwapendelea Ethiopia na hata wachezaji wa Zanzibar walipojaribu kulalamika waliishia kufokewa.
  Kwa kipigo cha leo, Zanzibar inabaki na pointi zake tatu ilizovuna kwa kuifunga Sudan Kusini 2-1 katika mchezo wa ufunguzi na Ethiopia iliyoanza kwa sare ya bila kufungana na wenyeji Kenya, inakuwa na pointi nne.
  Kikosi cha Zanzibar leo kilikuwa; Abdallah Rashid Abdallah, Adeyoum Saleh Ahmed, Salum Khamis Bakari, Waziri Salum Omar, Shaffi Hassan Rajab, Mohamed Fakhi Khatib, Sabri Ali Makame, Masoud Ali Mohamed/Isihaka Othman Omar dk87, Ali Badru Ali, Suleiman Kassim Suleiman ‘Selembe’/Seif Abdallah Rashid dk14 na Awadh Juma Issa.
  Ethiopia; Derete Aremu, Fasika Asfan, Salahadin Balgicho, Thok James, Moges Tedese, Shimekit Gugsa, Mulualem Mesfin, Mintesnote Adane, Yousuf Yassin Salah/Yonathan Kedebe dk64, Mehary Mena na Manaye Fantu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZANZIBAR YAPIGWA NA WAHABESHI NYAYO CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top