• HABARI MPYA

    Wednesday, April 10, 2019

    AZIM DEWJI AITABIRIA SIMBA SC KUITUPA NJE TP MAZEMBE LIGI YA MABINGWA AFRIKA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MFANYABIASHARA maarufu nchini aliyewahi kuifadhili timu ya soka ya Simba kwa mafanikio makubwa, Azim Dewji ameitabiria makubwa klabu hiyo katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwishoni mwa wiki hii huko mjini Lumbumbashi.
    Amesema Simba ya mwaka huu ni `moto’ na ina uwezo wa kuwang’oa Mazembe kutokana na kuundwa na wachezaji wenye vipaji na ari ya kupata matokeo chanya.
    Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Dewji aliyeifikisha Simba fainali za Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 1993, alisema kitu pekee kinachopaswa kufanywa na wachezaji na viongozi wa Simba ni kuondoa mchecheto wa mchezo na badala yake kuelekeza nguvu katika mchezo wa marudiano.
    Azim Dewji ameitabiria matokeo mazuri Simba SC katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe 

    “Ni kweli Mazembe ni timu ngumu na kongwe. Ukiangalia ina historia kubwa Afrika na ndani ya miaka hii kumi tumeshuhudia ikitwaa ubingwa tofauti wa michuano ya CAF mara tano.  Ni rekodi bora sana, lakini pamoja na ubora wao, nikiangalia ubora na uthubutu wa wachezaji wa Simba, naona vijana wetu wanaweza kufanya kweli.
    “Wachezaji wa sasa wa Simba nawafananisha na wale wa enzi zile tunafika fainali CAF. Walikuwa wanajituma sana uwanjani. Na hawa ukiwaangalia wana kila kitu kinachoweza kuwaduwaza Mazembe kwao. Angalia walivyowakimbiza hapa Dar es Salaam, kwa kawaida Mazembe si wa kujiangusha hivyo, lakini uliona katika mchezo wa kwanza, walizidiwa sana ila bahati haikuwa kwa Simba.
    “Na hata hao wanaobeza penalti ya John Bocco watambue Simba hii ni moto wa kuotea mbali na usishangae kuona mpira umetangulia Lubumbushi na wachezaji wanakwenda kumalizia kazi ya kuandika historia zaidi kwa soka ya Tanzania,” alisema Dewji.

    Kumkataa mwamuzi
    Akizungumzia tukio la klabu hiyo kupinga kubadilishiwa mwamuzi wa mchezo wa marudiano dhidi ya Mazembe, alisema jambo hilo litawarejesha mchezoni wachezaji, lakini pia kuongeza umakini wa waamuzi katika mchezo huo.
    “Hata kama CAF hawatabadilisha uamuzi huo, mwamuzi aliyepangwa (Janny Sikazwe wa Zambia) atakuwa makini zaidi na kizuri ni kwamba hatataka kuharibu sifa zake zilizomwezesha kuchezesha michuano karibu yote mikubwa duniani. Amechezesha Kombe la Dunia mara mbili, Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili, pia fainali za Klabu Bingwa ya Dunia, achilia mbali hii michuano ya klabu Afrika,” alisema Dewji aliyewataka Watanzania kuendelea kuwaunga mkono wawakilishi hao wa taifa.
    Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, timu hizo hazikufungana, hivyo kuzifanya timu zote kuwa na nafasi ya kusonga mbele hatua ya nusu fainali, matokeo ya mwishoni mwa wiki yakiwa mwamuzi wa mwisho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZIM DEWJI AITABIRIA SIMBA SC KUITUPA NJE TP MAZEMBE LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top