• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 17, 2019

  SERENGETI BOYS YAGONGWA TENA, YACHAPWA 3-0 NA UGANDA AFCON U17 TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imeendelea kufanya vibaya kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17), baada ya leo pia kuchapwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Mabao yaliyoizamisha Serengeti Boys leo yamefungwa na Andrew Kawooya dakika ya 16, Ivan Asaba dakika ya 28 na Najib Yiga dakika ya 77. 
  Kwa kipigo cha pili mfululizo leo, sasa Serengeti Boys itahitaji miujiza kuweza kuingia Nusu Fainali iwapo itaifunga Angola kuanzia 3-0 na Uganda itafungwa na Nigeria si chini ya 3-0 kwenye mechi za mwisho ili ifuzu kwa wastani wa mabao. 
  Wachezaji wa Serengeti Boys wakilaumiana leo baada ya kufungwa na Uganda michuano ya AFCON U17
  Ivan Asaba akishangilia baada ya kuifungia bao la pili Uganda leo

  Katika mchezo uliotangulia, Nigeria iliichapa 1-0 Angola, bao pekee la mshambuliaji Olakunle Junior Olusegun kwa penalti dakika ya 21.
  Kwa ushindi huo, Nigeria iliyoichapa Tanzania 5-4 Jumapili, inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na hao hao Angola wenye pointi tatu baada ya kuifunga Uganda kwenye mchezo wa kwanza.
  Mechi za mwisho za Kundi A zitachezwa Aprili 20 Serengeti Boys ikimenyana na Angola Uwanja wa Taifa na Nigeria na Uganda Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam, zote zikianza Saa 10:00 jioni.
  Kesho kutakuwa na mechi za Kundi B, Cameroon na Morocco Saa 10:00 jioni na Senegal dhidi ya Guinea kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex.
  Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Shaaban Hassan, Omary Omary, Arafat Swakali, Alphonce Msanga, Edmund John, Kelvin John, Pascal Msindo, Ladaki Chasambi, Amiri Njeru, Edson Mshirakandi/Salumu Milinge dk58 na Morice Abraham/Agiri Ngoda dk67.
  Uganda; Jack Komakech, Kevin Ssekimbegga, Kasozi Samson, Kizito Gavin, Ssekajja Davis, Kawooya Andrew/Isma Mugulusi dk62, Kakaire Thomas, Asaba Ivan/John Alou dk86, Najib Yiga, Rogers Mugisha/Abdulwahid Iddi dk58 na Justine Opiro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAGONGWA TENA, YACHAPWA 3-0 NA UGANDA AFCON U17 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top