• HABARI MPYA

  Wednesday, April 17, 2019

  SIMBA SC YAREJEA NA MOTO LIGI KUU, YAICHAPA COASTAL UNION 2-1 MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  SIMBA SC imerejea kwa kishindo kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Shujaa wa Simba SC leo alikuwa ni mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere aliyefunga mabao yote mawili.
  Na kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 60 baada ya kucheza mechi 23, ingawa inabaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 66 za mechi 31 na Yanga SC pointi 74 za mechi 32.
  Meddie Kagere akipongezwa na wenzake baada ya kuifungia Simba mabao yote mawili leo

  Chipukizi Raizin Hafhid alianza kuifungia Coastal Union dakika ya kwanza tu akitumia makosa ya beki Erasto Edward Nyoni kuchanganyana na kipa wake, Aishi Manula.
  Kagere akaisawazishia Simba SC kwa penalti dakika ya 48 mshambuliaji mwenzake wa kigeni, Mganda Emmanuel Arlond Okwi kuangushwa na kipa Soud Abdallah kwenye boksi.
  Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC tangu asajiliwe kutoka Gor Mahia ya Kenya akafunga bao la pili na la ushindi dakika ya 68 baada ya kuwazidi mbio mabeki wa  Coastal Union.  
  Simba SC ilikuwa inacheza mechi ya kwanza tu tangu itolewe kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kufuatia kuchapwa 4-1 na TP Mazembe mjini Lubumbashi Jumamosi. 
  Coastal Union; Soud Abdallah, Miraj Adam, Adeyoum Ahmed, Bakari Mwamnyeto, Kennedy Kipepe, Hajji Ugando, Mtende Juma, Ayoub Lyanga, Raizin Hafidh, Andrew Simchimba na Said Jailan.
  Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Hassan Dilunga, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAREJEA NA MOTO LIGI KUU, YAICHAPA COASTAL UNION 2-1 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top