• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 13, 2019

  SIMBA SC YACHAPWA 4-1 NA MAZEMBE LUBUMBASHI NA KUTUPWA NJE LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SAFARI ya Simba SC katika Ligi ya Mabingwa Afrika imefikia tamati leo baada ya kuchapwa mabao 4-1 na wenyeji, Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali jioni ya leo Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kwa matokeo hayo Simba SC inatolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi ya wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, hivyo kushindwa kurudia rekodi yake ya mwaka 1974 kufika Nusu Fainali.  
  Katika mcheze wa leo uliochezeshwa na refa Janny Sikazwe, aliyesaidiwa na Romeo Kasengele wote wa Zambia na Berhe Tesfagiorgis O'michael wa Eritrea, hadi mapumziko TP Mazembe walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

  Lakini ni Simba SC waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili tu kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyemlamba chenga kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo baada ya pasi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na kufunga kiulaini.
  Mazembe ikasawazisha bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa beki wake Mzambia Kabaso Chongo aliyemalizia pasi ya mshambuliaji Jackson Muleka baada ya kona iliyochongwa na Tressor Mputu.
  Na Meschak Elia akaifungia Mazembe bao la pili dakika ya 38 kwa shuti la mguu wa kushoto akitumia makosa ya beki Mburkinabe wa Simba SC, Zana Coulibaly.
  Kipindi cha pili, kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick Aussems akaanza na mabadiliko mfululizo akiwatoa beki Mganda Juuko Murshid na kiungo Muzamil Yassin na kuwaingiza kiungo Mzambia Clatous Chama na mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere.
  Hayakuwa mabadiliko yenye manufaa kwa timu, kwani yaliwasaidia Mazembe kupata mabao mawili zaidi, wafungaji Tessor Mputu dakika ya 62 na Muleka dakika ya 75, huku kipa Aishi Salum Manula akifanya kazi ya ziada kuokoa michomo zaidi ya hatari.
  Simba SC inarejea Dar es Salaam usiku wa leo kuelekeza nguvu zake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili iweze kutetea taji lake na kupata tena nafasi ya kucheza michuano ya Afrika msimu ujao. 
  Kikosi cha TP Mazembe kilikuwa; Sylvain Gbohouo, Joseph Ochaya, Issama Mpeko, Chongo Kabaso, Kevin Mondeko, Nathan Sinkala, Miche Mika, Rainford Kalaba/Koffi Christian dk76, Meschak Elia, Jackson Muleka na Tressor Mputu/Glody Likonza dk85.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Juuko Murshid/Clatous Chama dk53, Jonas Mkude, James Kotei, Muzamil Yassin/Meddie Kagere dk46, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi/Rashid Juma dk71 na John Bocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YACHAPWA 4-1 NA MAZEMBE LUBUMBASHI NA KUTUPWA NJE LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top