• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 18, 2019

  CAMEROON YAIFUATA NIGERIA NUSU FAINALI AFCON U17 2019 DAR

  TIMU ya taifa ya Cameroon imeungana na Nigeria kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Morocco kwenye mchezo wa Kundi B leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Hongera zake mfungaji wa mabao yote mawili ya Cameroon, mshambuliaji Ismaila Seidou dakika ya 73 na 90 na ushei akiiwezesha timu yake kutoka nyuma kufuatia Morocco kutangulia kwa bao la Tawfik Bentayeb dakika ya 22 na kupata ushindi wa pili kwenye mashindano.
  Cameroon sasa inafikisha pointi sita baada ya kuifunga na Guinea 2-0 kwenye mchezo wa kwanza, hivyo kuendelea kuongoza Kundi B, wakati Morocco inabaki na pointi yake moja, sawa na Senegal zikifuatana nafasi ya tatu na ya nne.
  Mechi nyingine ya Kundi B leo, Guinea imeichapa Senegal 2-1 na kupanda nafasi ya pili kwa pointi zake tatu kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya Morocco. Mabao ya Guinea yamefungwa na Algassime Bah dakika ya 33 na Momo Fanye Toure dakika ya 80, wakati la Senegal limefungwa na Samba Diallo dakika ya 10.
  Kesho ni mapumziko na mechi za mwisho za Kundi A zitachezwa Jumamosi, Tanzania na Angola Uwanja wa Taifa na Nigeria na Uganda Uwanja wa Azam Complex.
  Mechi za mwisho za Kundi B zitafuatia Jumapili, Guinea na Morocco Uwanja wa Taifa na Cameroon na Senegal Azam Complex. 
  Nigeria inaongoza Kundi A kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Uganda pointi tatu, Angola pointi tatu wakati wenyeji, Serengeti Boys wanashika mkia baada ya kufungwa mechi zote mbili za mwanzo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CAMEROON YAIFUATA NIGERIA NUSU FAINALI AFCON U17 2019 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top