• HABARI MPYA

  Sunday, April 21, 2019

  SERENGETI BOYS KAMA HAIKUWA NA MAANDALIZI AU BENCHI LA UFUNDI

  WENYEJI, Tanzania wametolewa kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa kupoteza mechi zote tatu za Kundi A Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Chini ya kocha Oscar Milambo, Serengeti Boys ilianza kwa kufungwa 5-4 na Nigeria kabla ya kuchapwa 3-0 na Uganda na jana ikahitimisha mechi zake za Kundi A kwa kuchapwa 4-2 na Angola, zote Uwanja wa Taifa. 
  Bahati bahati mbaya zaidi hata jirani zao, Uganda nao wametupwa nje baada ya sare ya 1-1 na Nigeria katika mchezo mwingine wa mwisho wa Kundi A Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam pia. 

  Maana yake, Nigeria iliyomaliza kileleni mwa kundi kwa pointi zake saba inaungana na Angola iliyomaliza na pointi sita kwenda Nusu Fainali na pia kujikatia tiketi ya fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Brazil.
  Katika mchezo wa jana, mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Omary Jumanne Omary dakika ya 12 na Agiri Aristides Ngoda dakika ya 44, wakati ya Angola yalifungwa na Telson Tome dakika ya 17, Osvaldo Capemba kwa penalti dakika ya 42, David Nzanza dakika ya 68 na Osvaldo Capemba dakika ya 72.
  Azam Complex kiungo John Kokas Alou alianza kuifungia Uganda dakika ya 69, kabla ya kiungo Ibraheem Olalekan Jabaar kuisawazishia Nigeria dakika ya 74.
  Mechi za mwisho za Kundi B zitachezwa leo Guinea na Morocco Uwanja wa Taifa na Cameroon na  Senegal Azam Complex na zote zitaanza Saa 10:00 jioni.
  Cameroon inaongoza Kundi B kwa pointi zake sita ikifuatiwa na Guinea yenye pointi tatu, wakati Morocco na Senegal kila moja ina pointi moja. 
  Kufanya vibaya kwa Serengeti Bosy ni kinyume na matarajio, kwani timu hiyo ilionyesha mwendelezo mzuri wakati wa maandalizi yake.
  Katika matayarisho yake, Serengeti Boys ilitwaa ubingwa wa Kombe la CECAFA Challenge U-17 baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Somalia Uwanja wa Ngozi mjini Bujumbura, Burundi Aprili 29 mwaka jana.
  Agosti 24 mwaka jana ikafungwa 3-2 na Uganda na kutolewa katika michuano ya kuwania tiketi ya kushiriki AFCON Qualifier 2019) Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. Agosti 26 ikashinda kwa penalti 4-3 dhidi ya Rwanda baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.
  Serengeti Boys ilitwaa ubingwa wa U17 Kanda ya Tano Afrika baada ya ushindi wa penalti 6-5 dhidi ya Angola kufuatia sare ya bao 1-1, kwenye mchezo wa fainali jana mjini Gaborone nchini Botswana Desemba mwaka jana.
  Ilishiriki michuano ya UEFA Assist nchini Uturuki na pamoja na kufungwa mechi mbili, 1-0 na Guinea na 5-0 na wenyeji, Uturuki huku ikishinda moja tu, 3-2 dhidi ya Australia lakini Serengeti Boys ilionyesha kiwango cha kuridhisha.
  Ikaenda kutwaa ubingwa wa michuano ya Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) baada ya sare ya mabao 3-3 na wenyeji na ushindi wa 2-1 dhidi ya Cameroon, hivyo kujikusanyia pointi nne na kuwapiku wapinzani.
  Cameroon iliyofungwa 3-2 na Serengeti Boys ni ambayo inaongoza Kundi B kwa sasa na ilitokea Rwanda moja kwa moja kuja kwenye AFCON U17 ikiwa timu ya kwanza kuwasili Dar es Salaam.
  Matokeo ya timu kwenye mashindano hayo yaliwajaza matumaini Watanzania kwamba timu yao itafanya vizuri na angalau kukata tiketi ya Kombe la Dunia kwa kufika Nusu Fainali kama si kuwa mabingwa.
  Lakini vipigo vitatu vimewaumiza Watanzania, wakiishuhudia timu yao ikicheza mpira mbovu na wazi lawama za kwanza ni za benchi la Ufundi.
  Kwa muda mrefu, Mwalimu Mkuu wa Serengeti Boys alikuwa Mdenmark Kim Poulsen na Milambo alikuwa Msaidizi wake.
  Hata hivyo, baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa CECAFA U17 nchini Burundi Poulsen aliondoka nchini na Milambo akapewa majukumu ya kocha Mkuu.
  Mawazo ya wengi juu ya kufanya vibaya kwa timu ni uwezo wa mwalimu, kwa sababu kwa ambao wamekuwa wakiifuatilia Serengeti Boys kwa karibu wanasema uwezo wa timu hiyo umekuwa ukishuka siku hadi siku tangu kuondoka kwa Poulsen Julai mwaka jana.
  Lakini pengine kutokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutingwa na mambo mengi, maandalizi ya fainali zenyewe za AFCON U17 na mechi za timu ya wakubwa, Taifa Stars kufuzu AFCON ya mwaka huu, Misri ufuatiliaji wa mwendendo wa Serengeti Boys haukuwepo tena, ama ulikuwa mdogo.
  Kiwango cha Serengeti Boys kwenye mashindano haya hakifanani na timu iliyoandaliwa kwa ajili ya mashindano, wakati maandalizi yalifanyika na ya muda mrefu. Kuna tatizo. Timu imetuumbua wote tuliojiweka kifua mbele kuamini itatuoa kimasomaso.
  Imecheza ovyo na kupoteza mechi zote, hivyo kutolewa mapema tu na baadaye ndipo kocha Milambo anasema wamefanya vibaya kwa sababu hawakuwa na maandalizi mazuri.
  Oscar ni kocha anayeinukia vizuri na ambaye kama atakuwa na mwendelezo mzuri anaweza kuwa mwalimu mzuri zaidi baadaye.
  Lakini kuwa kupewa majukumu yaliyomzidi uwezo mapema imemharibia na anahitaji ujasiri mkubwa kusimama imara na kuendelea, kwa sababu tayari wananchi hawamuhesabu tena kama kocha mzuri.
  Mwisho wa siku tusameheane tu na kujifunza kutokana na makosa, kwa sababu mpira wa miguu ni mchezo wa makosa amabyo yanaanzia kwa viongozi wa TFF, benchi la Ufundi na wachezaji wenyewe. Tujipange kwa mashindano yajayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS KAMA HAIKUWA NA MAANDALIZI AU BENCHI LA UFUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top