• HABARI MPYA

  Friday, April 26, 2019

  TAIFA STARS KUJIPIMA NA MISRI JUNI 13 MJINI ALEXANDRIA MAANDALIZI YA AFCON 2019

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza mchezo wa kirafiki na Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema kwamba huo utakuwa mchezo muhimu kwa kocha Emmanuel Amunike kupata taswira ya kikosi chake kabla ya mashindano kuanza. 
  Taifa Stars imepangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal, wakati Misri ambao ni wenyeji wapo Kundi A pamoja na na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Taifa Stars imefuzu AFCON ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
  Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
  Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS KUJIPIMA NA MISRI JUNI 13 MJINI ALEXANDRIA MAANDALIZI YA AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top