• HABARI MPYA

  Sunday, April 14, 2019

  MSUVA AMPIGIA HESABU SADIO MANE AFCON, ASEMA ATAMUONYESHA YEYE NI NANI MISRI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva amesema kwamba ana hamu ya kukutana na mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane kwa sababu amekuwa akimpenda sana mchezaji huyo wa Senegal. 
  Tanzania imepangwa Kundi C katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri pamoja na Kenya, Algeria na Senegal.
  Katika droo iliyoongoza na magwiji wa Afrika, Mustapha Hadji wa Morocco, Ahmed Hassan wa Misri, El Hadji Diouf wa Senegal na Yaya Toure wa Ivory Coast usiku wa jana ukumbi wa Sphinx & the Pyramids mjini Giza, wenyeji, Misri wamepangwa Kundi A pamoja na Zimbabwe, Uganda na DRC.
  Simon Msuva amesema ana hamu ya kukutana na Sadio Mane (pichani chini) kwenye AFCON ya Misri

  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, wakati Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F linazikutanisha Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kutoka Morocco anakochezea klabu ya Difaa Hassan El-Jadidi Msuva amesema kwamba nchini Morocco amekuwa akifananishwa na Mane kiasi cha wengine kumuita jina hilo.
  “Ndiyo, pacha wangu huyo (Sadio), kwa kweli niliapa katika maisha yangu ipo siku nitakutana naye uwanjani na sasa tumekutana, nadhani atanijua vizuri kama mimi ndiyo Msuva na Watanzania wapiganaji,”amesema.
  Msuva amesema Kundi C litakuwa na ushindani mkubwa kwenye AFCON kwa sababu linawakutanisha Taifa Stars na timu zenye wachezaji wengi wanaocheza Ulaya.
  “Kenya pia siwezi kuwabeza kwa sababu na wao wana wachezaji wanaocheza Ulaya, hivyo ushindani utakuwa mkubwa,”ameongeza.
  Taifa Stars ilifuzu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
  Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
  Taifa Stars itaanza na Senegal Juni 23 Saa 1:00 usiku, kabla ya kumenyana na Kenya Juni 27 Saa 4:00 usiku Uwanja wa Juni 30 na kumaliza na Algeria Julai 1 Saa 3:00 usiku Uwanja wa Al Salam mjini Cairo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA AMPIGIA HESABU SADIO MANE AFCON, ASEMA ATAMUONYESHA YEYE NI NANI MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top