• HABARI MPYA

  Sunday, April 14, 2019

  SERENGETI BOYS YAANZA VIBAYA MICHUANO YA AFCON U17, YACHAPWA 5-4 NA NIGERIA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WENYEJI, Tanzania wameanza vibaya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U-17) baada ya kuchapwa mabao 5-4 na Nigeria katika mchezo wa ufunguzi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni ya leo.
  Sasa kikosi cha kocha Oscar Rabson Mirambo kina kazi ya kuupanda mlima kwa kuhakikisha kinashinda mechi zake mbili zijazo dhidi ya Angola na Uganda ili kuwania tiketi ya Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Brazil.
  Hadi mapumziko, Nigeria inayofundishwa na kocha mzalendo pia, Manu Garba ilikuwa mbele kwa mabao 3-1.

  Mshambuliaji wa Tanzania, Kelvin Pius John akimtoka beki wa Nigeria, Shedrack Tanko

  Mabao ya Nigeria yalifungwa na Olatomi Olaniyan dakika ya 21, Wisdom Onyedikachi Ubani  dakika ya 30 na Akinkunmi Amoo dakika ya 37, wakati la Tanzania lilifungwa na Edmund John dakika ya 22.
  Na kipindi cha pili Tanzania ikazinduka na kusawazisha mabao hayo kupitia kwa Kelvin John dakika ya 52 na Morice Abraham kwa penalti iliyombabatiza kipa Suleiman Shaibu kabla ya kutinga nyavuni. 
  Edmund John akaifungia bao la nne Tanzania dakika ya 60 kwa penalti, lakini makosa ya kipa wa Serengeti Boys, Mwinyi Yahya yakawazawadia Nigeria mabao mawili rahisi yaliyofungwa na Wisdom Ubani dakika ya 72 kwa shuti la mpira wa adhabu na Ibraheem Jabaar dakika ya 78.
  Mchezo mwingine wa Kundi A kati ya Angola na Uganda unafuatia hivi sasa na kesho kutakuwa na mechi za Kundi B kati ya Guinea na Cameroon Saa 10:00 jioni na Morocco na Senegal Saa 1:00 usiku na zote zitaonyeshwa na ZBC 2.
  Serengeti Boys yenyewe itarejea uwanjania Jumatano kumenyana na Uganda Saa 1:00 usiku kabla ya kukamilisha mechi zake za Kundi A kwa kukipiga na Angola Jumamosi Saa 10:00 jioni hapo hapo Uwanja wa Taifa.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Mwinyi Yahya, Arafat Swakali, Mustapha Nankuku, Alphonce Msanga, Misungwi Chananja/Edson Mshirakandi dk34, Edmund John, Kelvin John, Pascal Msindo, Dominic William, Ally Rutibinga na Morice Abraham/Ladaki Chasambi dk82.
  Nigeria; Suleman Shaibu, Shedrack Tanko, Ogaga David Oduko, Samson Tijani, Clement Ferdinard Ikenna, David Ishaya, Olakunle Olusegun, Mayowa Abayomi/Fawaz Abdullahi dk80, Wisdom Onyedikachi Ubani, Akinkunmi Amoo na Olatomi Olaniyan/Ibraheem Jabaar dk71.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAANZA VIBAYA MICHUANO YA AFCON U17, YACHAPWA 5-4 NA NIGERIA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top