• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 20, 2019

  KAGERA SUGAR WAENDELZEA UBABE KWA SIMBA SC, WAICHAPA MABAO 2-1 UWANJA KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  TIMU ya Kagera Sugar imeendeleza ubabe wake kwa Simba SC baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Ushindi huo unaifanya Kagera Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ifikishe pointi 41 baada ya kucheza mechi 33 na kujiinua hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya timu 20 kutoka ya 17.
  Mabingwa watetezi, Simba SC wenyewe wanabaki nafasi ya tatu na pointi zao 64 katika mchezo wa 24, wakiwa nyuma ya Azam FC yenye pointi 66 na Yanga SC pointi 74 baada ya wote kucheza mechi 32.

  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, Kagera Sugar ilipata mabao yake yote mawili kipindi cha kwanza. 
  Alianza chipukizi, Kassim Hamisi kufunga dakika ya 17 kwa shuti ndani ya boksi akimalizia krosi ya mshambuliaji mwenza, Ramadhani Kapera kutoka pembeni kushoto baada ya kugongewa pasi na kiungo Venence Ludovic.
  Akafuatia Kapera mwenyewe kufunga dakika ya 41 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Ally Ramadhani aliyegongeana kona fupi na beki wa kushoto David Luhende.
  Kipindi cha pili kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick Aussems akaanza na mabadiliko, akimpumzisha kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima na kumuingiza mshambuliaji na Nahodha wa timu, John Raphael Bocco.  
  Bocco akakaribia kufunga dakika ya 52 baada ya kupiga kichwa na mpira kwenda juu kidogo ya lango kufuatia krosi ya beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi ambaye leo alikuwa chini ya ulinzi mkali wa beki Juma Said Nyosso akaifungia Simba SC bao pekee leo dakika ya 63 akimalizia krosi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama kutoka upande wa kulia.
  Beki Muivory Coast ambaye kwa mara nyingine mabao ya leo yamepitia upande wake, akapiga juu ya lango dakika ya 79 akiwa amebaki na kipa Said Khatib Kipao baada ya pasi nzuri ya kiungo Hassan Dilunga.
  Bocco naye tena dakika ya 84 akapiga shuti zuri la juu, lakini kwa mara nyingine Kipao akadaka kwa uhodari na refa Adongo akaongeza dakika tano na kuupeleka mchezo kwa dakika saba zaidi huku jitihada za Simba kupata japo bao la kusawazisha zikigonga ukuta. 
  Nafasi nzuri ya mwisho Simba walipata dakika ya 90+4 na Okwi akapiga kichwa juu ya lango akiwa kwenye boksi yeye na Kipao baada ya krosi ya kiungo Jonas Gerald Mkude iliyoparazwa na mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere ambaye leo hakuwa katika ubora wake.
  Huo unakuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Kagera Sugar dhidi ya Simba SC katika Ligi Kuu baada ya Mei 19 mwaka jana kushinda 1-0 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na aliyetoa usemi uliogeuka maarufu ‘Kagera wametoboa tundu la Simba’.
  Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Said Kipao, Mwaita Gereza, David Luhende, Juma Shemvuni, Juma Nyosso, Peter Mwalyanzi, Paul Ngalyoma/Majjid Hamisi dk74, Ally Ramadhani, Ramadhani Kapera/Hamad Waziri dk89, Kassim Hamisi na Venence Ludovic/Suleiman Mangoma dk87.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Erasto Nyoni, James Kotei/Hassan Dilunga dk56, Haruna Niyonzima/John Bocco dk46, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clatous Chama.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR WAENDELZEA UBABE KWA SIMBA SC, WAICHAPA MABAO 2-1 UWANJA KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top