• HABARI MPYA

  Friday, April 26, 2019

  ZAHERA AWAANDAA YANGA B KUIVAA AZAM FC BAADA YA ‘MAFAZA’ KUENDELEZA MGOMO LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga SC, Mwinyi Zahera leo amewafanyisha mazoezi wachezaji wa timu ya vijana, maarufu kama Yanga B kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu, kufuatia wachezaji wa kikosi cha kwanza kuendeleza mgomo.
  Kwa siku ya pili leo, wachezaji wa Yanga SC wamegoma kufanya mazoezi wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao pamoja na fedha za usajili.
  Mgomo huo ulianza asubuhi Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam wakati wachezaji walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.
  Mwinyi Zahera (katikati) leo amewafanyisha mazoezi wachezaji wa Yanga B kuelekea mchezo dhidi ya Azam FC Jumatatu 

  Wachezaji wote walifika mazoezini mapema Saa 2:00 asubuhi ya jana, lakini wakawaagiza Manahodha wao, Ibrahim Ajibu na Juma Abdul waende kumuambia kocha Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwamba hawatafanya mazoezi kwa sababu viongozi wamewapuuza.
  Na hiyo ni baada ya jana wachezaji hao kumuomba Zahera ambaye pia ni kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC awaite viongozi kwenye mazoezi ya leo asubuhi ili wajadiliane juu ya stahiki zao.
  Lakini kitendo cha kutotokea kwa kiongozi hata mmoja mazoezini jana kiliwaudhi wachezaji na kukubaliana kuondoka bila kufanya mazoezi.
  Na Kocha Zahera alionyesha msimamo wa kutotaka kujadiliana chochote na wachezaji zaidi ya kuwaamrisha waingie uwanjani kufanya mazoezi. Mwishowe, wachezaji wakaondoka na kocha naye na Maafisa wake wa benchi la Ufundi wakaondoka kinyonge.
  Baadaye kocha Zahera alimuagiza Mratibu wa timu, Hafidh Saleh awatumie ujumbe wachezaji wote kuwaambia wasipofika mazoezini leo wajue ndiyo wamejiondoa kwenye timu moja kwa moja. Na hafidh aliwatumia ujumbe wachezaji, lakini nao wakamjibu wanataka na viongozi wawepo leo.
  Leo wachezaji wamefika mazoezini kama kawaida, lakini hakukuwa na kiongozi hata mmoja zaidi ya Zahera na wasaidizi wake.
  Zahera alikuwa amekwishajiandaa kwa kuwaita wachezaji wa timu B na baada ya nyota wa kikosi cha kwanza kusistiza mgomo wao wa hadi wakutane na viongozi, Mkongo huyo akaendelea mazoezi na wachezjai wa timu ya vijana watupu.  
  Inaelezwa kwamba mgomo huu ni matokeo ya usaili wa wagombea kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa klabu Mei 5, mwaka huu.
  Ikumbukwe viongozi wote wa Yanga walijiuzulu kupisha uchaguzi Mkuu na Baraza la Wadhamini likaunda Kamati ya Usimamizi wa timu hadi uchaguzi utakapofanyika iliyohusisha viongozi waliokuwa madarakani.
  Mwenyekiti wa Kamati ni Lucas Mashauri, Makamu wake, Said Ntimizi na Wajumbe Hussein Ndama, Samuel Lukumay, Hussien Nyika, Moses Katabaro na Maulid Kitenge. 
  Lukumay na Nyika ndiyo walikuwa viongozi wa mwisho kujiuzulu Yanga na walikuwa wakishirikiana na Mashauri, Ntimizi na Ndama kwenye kuongoza timu.
  Mashauri alichukua fomu ya kuwania Uenyekiti, Lukumay Umakamu, Ntimizi na Nyika Ujumbe, lakini wote wakaenguliwa katika usajili kwa sababu mbalimbali.
  Inachukuliwa kama watu hao wameamua kujivua majukumu ya kuendesha timu baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na sasa mzigo unawaangukia wajumbe wengine, Katabaro na Kitenge ambao hata hivyo hawajawahi kuonekana japo mazoezini tangu wateuliwe.
  Na kinachowaumiza zaidi wachezaji ni kuona zoezi la kuichangia klabu linaendelea vizuri, huku Kocha Zahera akielekeza nguvu zake kwenye kujenga kikosi cha msimu ujao wakati wao wana miezi mitatu hawajalipwa mishahara na wengi wanadai fedha za usajili.
  Wachezaji wanalalamika kwamba hakuna hata usafiri wa kwenda mazoezini na hali zao binafsi ni mbaya kwa sababu hawana mishahara wala posho katika timu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZAHERA AWAANDAA YANGA B KUIVAA AZAM FC BAADA YA ‘MAFAZA’ KUENDELEZA MGOMO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top