• HABARI MPYA

  Tuesday, April 23, 2019

  SIMBA SC YAAMSHA HASIRA MWANZA, YAIPIGA ALLIANCE FC MABAO 2-0 CCM KIRUMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC wamezinduka na kuichapa Alliance FC mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Simba SC inafikisha pointi 63 baada ya kucheza mechi 25, ingawa inabaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 66 za mechi 32 na Yanga SC pointi 74 za mechi 32 pia.
  Mchezaji wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima alianza kuifungia Simba SC dakika ya 21 akituliza kifuani kwa ustadi mkubwa krosi ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin kabla ya kufumua shuti kali lililotinga nyavuni.    Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi akaifungia bao la pili Simba SC dakika ya 75 baada ya kuwatoka mabeki wa Alliance kabla ya kufumua shuti kufuatia pasi nzuri ya Niyonzima ambaye kwa sasa yuko katika kiwango kizuri mno.
  Okwi alifunga bao hilo kiasi cha dakika 10 tu tangu aingie uwanjani kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji chipukizi wa Tanzania, Adam Salamba. 
  Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco kwa mara nyingine leo hakuwa mwenye bahati baada ya kuanzishwa kabla ya kutolewa dakika 10 za mwisho kumpisha mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere. 
  Alliance leo walizidiwa kila idara na Simba SC ambayo kama wachezaji wake wangeongeza umakini katika kumalizia nafasi walizotengeneza wangeondoka na ushindi mnono zaidi.
  Kikosi cha Alliance FC kilikuwa; John Mwanda, Godlove Mdumule, Siraj Juma, Joseph James, Geoffrey Luseke, Juma Nyangi, Richard John/Hussein Javu dk29, Shaaban William/Samir Vincent dk73, Michael Chinedu/Bigirimana Blaise dk64, Balama Mapinduzi na Dickson Ambundo. 
  Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Yussuf Mlipili, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Hassan Dilunga/Clatous Chama dk57, Adam Salamba/Emmanuel Okwi dk64, John Bocco/Meddie Kagere dk80 na Haruna Niyonzima.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAAMSHA HASIRA MWANZA, YAIPIGA ALLIANCE FC MABAO 2-0 CCM KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top