• HABARI MPYA

  Thursday, April 25, 2019

  PAPY FATY AZIMIA UWANJANI NA KUFARIKI DUNIA ESWATINI

  KIUNGO wa kimataifa wa Burundi, Papy Faty amefariki dunia miezi mitatu kabla ya nchi yake kushiriki fainali zake za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kihistoria.
  Papy Faty alirejeshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa hivi karibuni baada ya miaka mitatu ya kukosekana na alitarajiwa kuwemo kwenye kikosi kitakachosafiri kwenda Misri katikati ya mwaka.
  Hata hivyo, miezi mitatu baada ya kuonywa na Madaktari juu ya matatizo yake ya muda mrefu ya moyo, Faty amefariki dunia leo jioni baada ya kuzimia wakati akiichezea klabu yake, Malanti Chiefs nchini Eswatini, zamani Swaziland.
  Faty alizimia uwanjani baada ya dakika 15 tu tangu mchezo uanze kabla ya kukimbizwa hospitali ambako alithibitishwa kufariki dunia.
  Faty alishauriwa na madaktari mwezi Januari mwaka huu kuacha kucheza soka kutokana na matatizo yake ya moyo, lakini akakaidi ushauri ingawa klabu yake ya wakati huo, Bidvest Wits ya Afrika Kusini ilimuacha.
  Akahamia Malanti, ambako alifunga mabao mawili katika mechi saba na kurejeshwa timu ya taifa na akakaa benchi muda wote wa mchezo, Burundi ikitoa sare ya 1-1 na Gabon na kukata tiketi ya AFCON ya mwaka huu Misri. 
  Kabla ya mchezo huo alikaririwa akisema matatizo yake ya moyo yamekwisha. “Siumwi tena [moyo] kabisa. Na kwa sababu ni mchezo wa mwisho na tunahitaji pointi moja kufuzu, hivyo wanahitaji wachezaji wazoefu na ambao wamekuwa wakiipigania timu kabla. Na ndiyo maana Shirikisho na kocha wameniita na waliulizia juu ya hali yangu. Nikawaambia ilivyo,”alisema.
  Burundi, ambayo inajivunia wachezaji wake wakubwa kama mshambulaji wa Stoke City, Saido Berahino na Gael Bigirimana wa Hibernian wamefanikiwa kufuzu AFCON kwa mara ya kwanza katika historia yao ambazo zitashirikisha timu 24 kutoka 16, ikiwa imepangwa Kundi B pamoja na Nigeria, Guinea na Madagascar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PAPY FATY AZIMIA UWANJANI NA KUFARIKI DUNIA ESWATINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top