• HABARI MPYA

    Saturday, April 27, 2019

    ‘KAPTENI’ BOCCO APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAITANDIKA BIASHARA UNITED 2-0 MUSOMA

    Na Mwandishi Wetu, MUSOMA
    SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Biashara United jioni ya leo Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
    Shujaa wa Simba SC leo ni Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote mawili kipindi cha kwanza.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji Patrick Aussems inafikisha pointi 69 baada ya kucheza mechi 27 na kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Yanga SC wenye pointi 74 za mechi 32.


    Bocco, mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, alifunga mabao yake yake yote akimalizia kazi nzuri ya beki Mghana, Asante Kwasi la kwanza dakika ya 33 kwa shuti baada ya pasi ndefu na la pili kwa kichwa akimalizia krosi kutoka upande wa kushoto.
    Refa Ally Simba kutoka Geita alimtoa kwa kadi nyekundu kiungo Mnyarwanda wa SImba, Haruna Niyonzima dakika ya 71 baada ya kumuonyesha kadi ya pili ya njano kwa kumtolea maneno machafu mwamuzi huyo.
    Haruna alifanya hivyo baada kuonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Juma Mpakala wa Biashara United na pamoja na kuonywa na Nahodha wake, Mganda Emmanuel Okwi alikaidi na kuendelea kujibizana na refa hadi akaadhibiwa tena kwa kadi nyekundu.
    Aussems alimtoa mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere na kumuingiza kiungo mzawa, Hassan Dilunga baada ya kadi hiyo nyekundu ili kuulinda ushindi wake.
    Simba SC inakamilisha mechi zake za nne za Kanda ya Ziwa ikikusanya pointi tisa baada ya ushindi dhidi ya Alliance FC na KMC mjini Mwanza ikitoka kufungwa 2-1 na Kagera Sugar mjini Bukoba.  
    Kikosi cha Biashara United kilikuwa;Nourdine Balora, Waziri Rashid/Tariq Seif dk56, Innocent Edwin, James Kihimba,  Derick Mussa, George Makanga/Juma Mpakala dk67, Taro Donald/Kauswa Bernard dk75, Lenny Kissu, Mpapi Nassibu, Lameck Chamkaga na Geoffrey Malibiche.
    Simba SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Asante Kwasi/Yussuf Mlipili dk85, Paul Bukaba, Juuko Murshid, Said Ndemla, Haruna Niyonzima, Muzamil Yassin, John Bocco/Emmenuel Okwi dk58, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk74 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ‘KAPTENI’ BOCCO APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAITANDIKA BIASHARA UNITED 2-0 MUSOMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top