• HABARI MPYA

    Monday, April 16, 2018

    SIMBA SC YAZIDI KUUKARIBIA UBINGWA, YAIPIGA PRISONS 2-0 TAIFA…OKWI NA BOCCO WAENDELEA KUTISHA KWA MABAO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imezidi kupiga kasi kuelekea lilipo taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Gasper Ketto wa Arusha na Kassim Safisha wa Pwani, Simba ilipata bao moja kila kipindi cha wafungaji ni wale wale vinara wake wa mabao, washambuliaji Mganda Emmanuel Okwi na mzawa John Bocco.
    Ushindi huo unaifanya Simba SC yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam ifikishe pointi 58 baada ya kucheza mechi 23, sasa ikiwazidi kwa pointi 11 mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi. 

    Emmanuel Okwi (kushoto) akishangilia na John Bocco (kulia) baada ya bao la kwanza leo
    Beki wa Prisons, Nurdin Chona akijaribu kuupitia mpira miguuni mwa Emmanuel Okwi (kulia)
    Mshambuliaji wa Simba, John Bocco akipasua katikati ya wachezaji wa Prisons
    Winga wa Simba SC, Shiza Kichuya akiwatoka wachezaji wa Prisons leo 
    Beki wa Prisons, Salum Kimenya akimuacha chini beki wa Simba, Mghana Asante Kwasi

    Nahodha John Raphael Bocco aliye katika msimu wake wa kwanza tangu awasili kutoka Azam FC alifunga bao lake la 14 msimu huu dakika ya 35 kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la beki Erasto Edward Nyoni.
    Tanzania Prisons walikuja juu baada ya bao hilo na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Simba SC kusaka bao la kusawazisha, lakini kipa namba moja nchini, Aishi Salum Manula akadhihirisha ubora wake kwa kuokoa hatari zote.
    Prisons walipata pigo dakika mbili kabla ya mchezo kuwa mapumziko, baada ya mchezaji wake, Cleophace Mkandala kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Ramadhani ibata.
    Kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na kocha Mfaransa, Pierre Lechantre, anayesaidiwa na Mtunisia, Aymed Mohammed Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzawa Muharammi Mohammed ‘Shilton’, kocha wa makipa  ilirudi vizuri na kuanza kusaka mabao ya kuunenepesha ushindi wake, ingawa Prisons walikuwa wagumu kukubali mapema.
    Jutihada za Simba zilizaa matunda dakika ya 80 baada ya Mganda, Emmanuel Arnold Okwi kufunga bao lake la 19 la msimu kwa penalti kufuatia Nahodha Bocco kuchezewa rafu kwenhye boksi na refa wa Kigoma, Shomary Lawi kutenga tuta hilo.
    Bao hilo liliwavunja nguvu Tanzania Prisons ambao kutoka hapo walianza kucheza kwa kujizuia kuruhusu mabao zaidi. 
    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Kagera Sugar imetumia vyema Uwanja wa nyumbani, Kaitaba mjini Bukoba kwa kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mabao yake yote yakifungwa na Jaffar KIbaya dakika za 45 na 53, huku la wageni likifungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 26.
    Nayo Ruvu Shooting imeibuka na ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Nicholaus Gyan dk85, Juuko Murshid, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Asante Kwasi, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo dk85, John Bocco na Shiza Kichuya. 
    Tanzania Prisons: Aaron Kalambo, Benjamin Asukile, Leonsi Mutalemwa, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Salum Kimenya, Cleophace Mkandala/Ramadhani ibata dk43, Mohammed Rashid, Freddy Chudu/John Sungura dk82 na Eliuter Mpepo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAZIDI KUUKARIBIA UBINGWA, YAIPIGA PRISONS 2-0 TAIFA…OKWI NA BOCCO WAENDELEA KUTISHA KWA MABAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top