• HABARI MPYA

  Tuesday, April 17, 2018

  MECHI YA LIPULI NA SIMBA SC UWANJA WA SAMORA YASOGEZWA MBELE KWA SIKU MOJA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BODI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeusogeza mbele kwa siku moja mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji, Lipuli na Simba SC kutoka Aprili 20 hadi 21, mwaka huu. 
  Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi, Boniphace Wambura Mgoyo kwa klabu zote, Lipuli na Simba, Msimamizi wa Kituo cha Iringa, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Kamisaa wa Mechi, Kamati ya Waamuzi na Wadhamini, imesema kwamba sababu ya kuuahirisha mchezo huo ni Uwanja wa Samora mjini Iringa na kuwa na matumizi mengine Aprili 20.
  “Sababu za mabadiliko hayo ni wamiliki wa Uwanja huo kuutumia kwa shughuli nyingine ya kijamii,”imesema taarifa ya Bodi, ikisitiza waliotumiwa wote kuzingatia mabadiliko hayo.

  Kocha wa Lipuli ya Iringa, Suleiman Matola atakutana na timu yake ya zamani Aprili 21 

  Wakati huo huo, taarifa zinasema Simba SC itaondoka asubuhi ya Jumanne kwenda Iringa tayari kwa mchezo huo.
  Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo, ikitoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jioni ya Jumatatu katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Gasper Ketto wa Arusha na Kassim Safisha wa Pwani, Simba ilipata bao moja kila kipindi cha wafungaji ni wale wale vinara wake wa mabao, washambuliaji Mganda Emmanuel Okwi na mzawa John Bocco.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam ifikishe pointi 58 baada ya kucheza mechi 23, sasa ikiwazidi kwa pointi 11 mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI YA LIPULI NA SIMBA SC UWANJA WA SAMORA YASOGEZWA MBELE KWA SIKU MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top