• HABARI MPYA

    Sunday, April 15, 2018

    AZAM FC YAISAIDIA POINTI MOJA NJOMBE MJI FC INAYOPIGANA KUEPUKA KUSHUKA DARAJA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Njombe Mji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Sare hiyo inaiongezea pointi moja Azam FC na kufikisha 46 baada ya kucheza mechi 25, wakati Njombe Mji FC inafikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 25 pia na kuendelea kushika mkia.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Malimi Busungu dakika ya 17 lilitosha kuipa ushindi wa 1-0 Lipuli ya Iringa dhidi ya Singida United Uwanja wa Samora.
    Katika mechi ya mahasimu wa Mji wa Shinyanga, Stand United wameibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex. Mabao ya Stand United yamefungwa na Tariq Seif dakika ya 51, Suleiman Ndikumana dakika ya 61 na Sixtus Sabilo dakika ya 75.
    Mbao FC imelazimishwa sare ya 2-2 na Maji Maji ya Songea Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Mabao ya Mbao yamefungwa na Boniphace Maganga yote mawili dakika ya 60 na 62, wakati ya Maji Maji yamefungwa na Marcel Kaheza dakika ya 81 na 90.
    Maji Maji inaendelea kushika nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu ya timu 16, ikifikisha pointi 20 baada ya kucheza mechi 15, nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 23 za mechi 24 sawa kabisa na Ndanda FC ya Mtwara.
    Stand United inapanda kwa nafasi mbili hadi ya tisa, ikifikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 25, wakati Mwadui FC inabaki nafasi ya 10 kwa pointi zake 26 za mechi 25.     
    Ligi Kuu itaendelea kwa mchezo mmoja tu kesho, vinara Simba SC wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
    Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 55 za mechi 23, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 za mechi 22.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAISAIDIA POINTI MOJA NJOMBE MJI FC INAYOPIGANA KUEPUKA KUSHUKA DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top