• HABARI MPYA

    Wednesday, March 07, 2018

    LEO NI ZAMU YA SIMBA NA WAARABU TAIFA BAADA YA YANGA ‘KUTIA AIBU’ JANA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC inateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni ya leo kumenyana na Al Masry ya Misri katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
    Mchezo huo utakaoanza Saa 12:00 jioni ili kuwapa fursa watazamaji wengi kujitokeza uwanjani baada ya pilika za kutwa za kujitafutia riziki, unatarajiwa kuwa na ushindani mkali.
    Hiyo inatokana na timu zote kukutana zikiwa katika viwango vizuri na pia zina wachezaji bora, damu mchanganyiko kwenye vikosi vyao kuanzia vijana wadogo na wakubwa wenye uzoefu.
    Simba ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre imefika hatua hii baada ya kuitoa Gendarmerie Tnare kwa jumla ya mabao 5-0 ikishinda 4-0 Dar es Salaam na kwenda kushinda 1-0 Djibouti City, wakati Al Masry ya kocha mzalendo, Hossam Hassan iliing’oa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 5-2, ikishinda 4-0 Cairo na kwenda kufungwa 2-1.  
    Baada ya matoeko hayo katika Raundi ya Awali ya mashindano, sasa timu bora zinazofanya vizuri hadi kwenye Ligi Kuu za nchini mwao zinakutana katika Raundi ya Kwanza.  
    Kocha Lechantre aliyejiunga na Simba SC Januari tu kuchukua nafasi ya Mcameroon, Joseph Marius Omog anaanini timu yake iko tayari kwa changamoto dhidi ya Al Masry.
    Lechantre amesema wachezaji wake wako vizuri na anatarajia watapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa leo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo. 
    Nahodha John Raphael Bocco alisema jana kwamba pamoja na ubora wa wapinzani wao, Al Masry, lakini watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo.
    Simba SC imekuwa kambini katika hoteli ya Sea Scape Kunduchi, Dar es Salaam ikifanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani tangu baada ya mchezo dhidi ya Stand United ya Shinyanga wakitoa sare ya 3-3 katika Ligi Kuu Ijumaa iliyopita.
    Al Masry wapo Dar es Salaam tangu Jumamosi na wamefikia katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski huku wakifanya mazoezi Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.   
    Kila la heri Simba SC. Mungu ibariki Simba, Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LEO NI ZAMU YA SIMBA NA WAARABU TAIFA BAADA YA YANGA ‘KUTIA AIBU’ JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top