• HABARI MPYA

    Monday, February 05, 2018

    POLISI MARA YAREJEA LIGI KUU KAMA BIASHARA UNITED MIAKA 15 TANGU ITEREMKE CHINI YA KIBADENI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE mkoa wa Mara utakuwa na timu tena katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya miaka 15 kufuatia Biashara United kumaliza nafasi ya kwanza katika Kundi B jana Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
    Ushindi wa mabao 3-2 wa Biashara United dhidi ya Transit Camp jana Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara unaipandisha Ligi Kuu timu hiyo baada ya kumaliza na poini 30, ikifuatiwa na Alliance Schools iliyomaliza na pointi 28 kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Oljoro jana Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
    Mjini Musoma; Mabao ya Biashara United yalifungwa na Sospeter Maiga Mandala dakika ya 59 kwa penalti baada ya mshambuliaji Songa Bethel aliyefunga la pili dakika ya 79 kuchezewa rafu kwenye boks na la tatu lilifungwa na Mohamed Soud dakika ya 85, wakati ya Transit Camp yote yalifungwa na Hussein Mgate dakika ya 44 na 90.
    Mjini Mwanza jana mabao ya Alliance yalifungwa na Dickson Ambundo dakika ya 15 kwa penalti baada ya mshambuliaji Athanas Mdamu aliyefunga bao la pili dakika ya 47, kuangushwa kwenye boksi na JKT Oljoro ikapata bao lake kupitia kwa Kuha Fabian dakika ya 83.
    Biashara United inarejea Ligi Kuu miaka 15 baadaye tangu ishuke enzi hizo ikijulikana kama Polisi bado

    Kwa mara ya kwanza Mara ilipandisha timu Ligi Kuu mwaka 2003, ambayo ilikuwa ni Polisi Mara chini ya kocha gwiji, Abdallah Athumani Seif ‘King KIbadeni’, lakini ikateremka baada ya msimu huo mmoja tu na sasa Biashara United, ambayo ndiyo ilikuwa Polisi Mara inarudi tena miaka 15 baadaye.
    Ni mwaka jana tu jeshi la Polisi mkoani Mara lilipoiacha timu hiyo na kuchukuliwa na wadau wa soka mkoani humo walioisimamia vyema hadi sasa inarejea Ligi Kuu.
    Dodoma FC ya kocha Jamhuri Kihwelo iliyopewa nafasi kubwa ya kupanda, imeikosa Ligi Kuu pamoja na ushindi wa 2-0 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Mgambo mkoani Dodoma jana mabao ya Jamal Machelanga dakika ya 84 na Anuari Jabir dakika ya 88, tu kwa kuzidiwa wastani wa mabao (GD) na Alliance Schools, kwani nayo imemaliza na pointi 28.   
    Mechi nyingine ya kundi hilo jana, Rhino Rangers ilipokea kipigo cha 1-0 kutoka kwa Pamba ya Mwanza Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora.
    Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017-2018 inakamilishwa leo kwa mechi za Kundi A; Kiluvya United ikiwakaribisha African Lyon wa Filbert Bayi mkoani Pwani, Friends Rangers wakiwakaribisha Mvuvumwa Uwanja wa Azam Complex, JKT Ruvu wakiwakaribisha Mshikamano Uwanja wa Meja Isamuhuyo Mbweni na Ashanti wakiwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Ikumbukwe katika Kundi A, tayari JKT Tanzania, zamani JKT Ruvu imekwishapanda baada ya kufikisha pointi 34 na sasa inaziachia kimbenbe African Lyon yenye pointi 24 na Friends Rangers yenye pointi 22 kugombea nafasi ya mwisho kupanda kutoka kundi hilo.
    Kundi C tayari nalo limekamilisha timu zake mbili za kupanda Ligi Kuu, ambazo ni KMC ya Kinondoni iliyomaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake 28 na Coastal Union ya Tanga iliyomaliza na pointi 26 wakizipiku JKT Mlale pointi 25 na Polisi Tanzania pointi 24.
    Timu mbili zinapanda kutoka kila kundi na kufanya idadi ya timu sita kwenda Ligi Kuu, ambako timu mbili zitashuka mwishoni mwa msimu katikati ya mwaka – ili kupata timu 20 za Ligi Kuu ya msimu ujao wa 2018-2019.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POLISI MARA YAREJEA LIGI KUU KAMA BIASHARA UNITED MIAKA 15 TANGU ITEREMKE CHINI YA KIBADENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top