• HABARI MPYA

  Sunday, January 14, 2018

  WAKATI UMEFIKA SASA PENGO LA MANJI LIZIBWE YANGA

  KLABU ya Yanga imekuwa haina Mwenyekiti tangu Mei mwaka jana, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji.
  Kwa kipindi chote hicho, Clement Sanga amekuwa akikaimu nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo, hata ikampa hadhi ya kugombea Uenyekiti wa Bodi ya Ligi, aliofanikiwa kushinda.
  Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
  Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji atakumbukwa kwa mengi – kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
  Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
  Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
  Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
  Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
  Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
  Na ni katika kipindi hicho ilishuhudiwa Manji aliwazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
  Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
  Julai 16, mwaka 2012 Manji akaamua kuingia kuongoza mwenyewe Yanga, baada ya kuona watu aliowasapoti wawe viongozi kuanzia Wakili Imani Omar Madega na Nchunga hawafanyi vile wanavyotaka.
  Manji akashinda kwenye uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za viongozi waliojuzuliu, akikusanya kura 1876, akifuatiwa kwa mbali na John Jembele aliyepata kura 40 na Edgar Chibura kura nne.
  Sanga akashinda nafasi ya Umakamu Mwenyekiti kwa kura 1948, akiwazidi Yono Kevela aliyepata kura 475 na Ayoub Nyenzi kura 288, wakati Abdallah Bin Kleb (kura 1942), Moses Katabaro (kura 1068),  Aaron Nyanda (kura 922) na Geroge Manyama (kura 682) wakashinda Ujumbe wa Kamati ya JUtendaji.
  Baada ya uongozi wa Manji kumaliza muda wake, katika uchaguzi wa Juni 11, mwaka 2016 baadhi ya watu muhimu kama Bin Kleb hawakutaka kurejea kutokana na sababu mbalimbali. Manji na Sanga wakarejea kwa ushindi wa kishondo.
  Mapema mwaka 2017, Manji aliwasilisha mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
  Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
  Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu kabla ya kujiuzulu Mei mwaka jana.
  Baadaye Manji akawekwa rumande gereza la Keko kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kipindi hicho ikashuhudiwa Yanga wakiwa naye bega kwa began a kumsaidia kujinasua kwenye kesi hiyo, hatimaye kufutiwa mashitaka.
  Kumekuwa na matumaini ya Manji atarejea na hayo ndiyo yamekuwa wakiwafanya wanachama wa Yanga wasihoji uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyoachwa na mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasi.
  Lakini bado Yanga ni klabu inayoongozwa kwa misingi ya Katiba, ambayo haielekezi ukiukwaji kwa sababu yote – hivyo ni dhahiri suala la uchaguzi mdogo kujaza nafasi za viongozi walioondoka halikwepeki.
  Na ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo wakati wote limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Katiba za klabu hazivunjwi imekuwa kimya juu ya Yanga kutokuwa na Mwenyekiti kwa takriban mwaka mzima sasa.
  Hata huo mchakato wa mabadiliko ya kuendeshwa wa klabu unafanyika chini ya Katiba iliyopo ambayo inasiginiwa sasa kwa kuacha klabu iende bila Mwenyekiti kwa karibu mwaka sasa. Naamini wakati umefika sasa pengo la Manji lizibwe Yanga.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAKATI UMEFIKA SASA PENGO LA MANJI LIZIBWE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top