• HABARI MPYA

  Wednesday, January 10, 2018

  SHUGHULI PEVU NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI LEO, YANGA NA URA, AZAM NA SINGIDA

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  NYASI bandia za Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo zitahimili zaidi ya dakika 180 ngumu wakati wa mechi mbili za Nusu za Kombe la Mapinduzi.
  Yanga SC watakutana na URA ya Uganda katika Nusu Fainali ya kwanza Kombe la Mapinduzi Saa 10:30 jioni kabla ya Azam FC kuvaana na Singida United Saa 2:15 usiku hapo hapo Amaan.
  Yanga wameingia Nusu Fainali kama washindi wa pili wa Kundi B, baada ya kulingana kwa pointi na Singida United walioongoza kwa wastani wa mabao tu, kufuatia kila timu kushinda mechi nne na kutoa sare moja katika mchezo baina yao.
  URA wameongoza Kundi A baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, wakifuatiwa na Azam waliopoteza mechi moja mbele ya timu hiyo ya Uganda na kushinda nyingine zote tatu.
  Viungo tegemeo wa Singida United, Deus Kaseke (kulia) na Mudathir Yahya wana kazi na Azam FC leo

  URA inapewa nafasi kubwa ya kuiangusha Yanga katika mchezo wa leo, kutokana na kuonekana kuwa na kikosi bora kuliko cha mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Lakini Yanga nayo inatarajiwa kuendeleza maajabu yake iliyoanza nayo kwenye hatua ya makundi, ambako haikupewa nafasi ya kufika popote ikipuuzwa kwamba haipo katika ubora unaohitajika kufanya vizuri kwenye mashindano.
  Mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua zaidi ni kati ya Azam FC na Singida United, timu pekee zilizobaki Tanzania zina makocha Wazungu.
  Mholanzi Hans van der Pluijm wa Singida United na Mromania Aristica Cioaba wa Azam FC kila mmoja atataka kudhihirisha ni zaidi ya mwenzake leo kuanzia Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan.
  Kila mmoja ana wachezaji wa chaguo lake kikosini baada ya usajili mzuri wa mapendekezo yao na wamiliki wa timu zao hawakuwabania fungu la kusajili yeyote waliyemtaka – tunasubiri kazi Amaan leo ili kupata timu za kukutana Fainali ya Mapinduzi Jumamosi usiku.   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHUGHULI PEVU NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI LEO, YANGA NA URA, AZAM NA SINGIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top