• HABARI MPYA

    Friday, January 19, 2018

    MASOUD JUMA: KIPIGO CHA SINGIDA JANA NI MAJIBU KWA WALIONIBEZA NA MFUMO WANGU

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KOCHA Msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Juma amesema kwaMBA, kutokana na ushindi mnono walioupata dhidi ya Singida United, alitaka kuwadhihirishia wale waliokuwa wanamkashifu juu ya mfumo wake mpya anaoutambulisha kwenye kikosi hicho.
    Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Singida walioibuka na ushindi wa mabao 4-0, Juma alisema, watu walitakiwa kuwa na subira kutokana na kile alichokuwa anafanya lakini badala yake walianza kuongea mengi.
    Alisema, mfumo wa 3-5-2 unahitaji wachezaji kujituma zaidi na wanapofika kwenye eneo la 18 kushambulia sana, lakini wachezaji walikuwa hawajazoea kutokana na kilikuwa kitu kipya kwao.
    Mrundi Masoud Juma (kushoto)  katika benchi la Ugfundi la Simba jana Uwanja wa Taifa 

    "Namshukuru Mungu kwa ushindi wa leo, haikuwa mechi rahisi, Singida ni timu nzuri na kocha wake namuheshimu sana kwa kazi yake, lakini matokeo haya ni kutokana na kutokata tamaa kwani watu waliongea sana juu ya mfumo mpya ndio maana timu ilifanya vibaya Mapinduzi lakini ilitakiwa uvumilivu," alisema Djuma.
    Akizungumzia juu ya ujio wa kocha mpya mkuu wa timu hiyo, Mfaransa, Pierre Lechantre aliyekuja na kocha wa mazoezi ya viungo, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi, Juma alisema kwanza anamkaribisha sana na anampa maelezo yote juu ya timu tangu alipoikuta na mabadiliko aliyofanya.
    Alisema baada ya hapo iwapo ataamua kuendelea na mfumo wa sasa alioanzisha yeye ni sawa na kama ataamua kubadilisha na kuja na falsafa yake yote kwake ni sawa.
    "Mimi sina tatizo kabisa, namkaribisha sana, nitampa maelezo yote ya timu tangu nimekabidhiwa na iwapo akiona inafaa kuendelea na mfumo wa sasa au kubadili na kuleta wake yote kwangu ni sawa," alisema Djuma.
    Baada ya matokeo hayo, Simba imeendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakijikusanyia pointi 29 na michezo 13 waliocheza wakifuatiwa na Azam nafasi ya pili wakiwa na pointi 27, nafasi ya tatu wakiwa Singida United na pointi 23 huku wapinzani wao Yanga wakiwa nafasi ya nne na pointi 22.
    Kocha Mholanzi Singida United, Hans van der Pluijm (kulia) akizungumza na Masoud Juma wa Simba jana kabla ya mechi

    Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Singida United, Mholanzi, Hans van der Pluijm, amesema kuwa licha ya kupoteza mchezo wa leo dhidi ya Simba, lakani sifa nyingi ni kwa timu yake kutokana na kujituma lakini bahati haikuwa upande wao.
    Singida ilikubali kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Simba, kwenye mchezo wa raundi ya 13 ya Ligi Kuu Bara, uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Pluijm alisema kuwa, anawapongeza sana Simba kwa ushindi huo mnono na kilichotokea ni matokeo ya mchezo hvyo atakwenda kufanya marekebisho ya makosa yao.
    "Unaweza kuona ni jinsi gani sina furaha leo, kilichotokea ni moja ya mchezo, vijana wangu walikuwa vizuri lakini bahati leo haikuwa yetu, tunahitaji kufanya kazi kubwa kurekebisha makosa," alisema Pluijm.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASOUD JUMA: KIPIGO CHA SINGIDA JANA NI MAJIBU KWA WALIONIBEZA NA MFUMO WANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top