• HABARI MPYA

    Monday, January 08, 2018

    ATHUMANI JUMA ‘CHAMA JOGOO’ AFARIKI DUNIA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Juma ‘Chama’ aliyeweika klabu za Pamba FC ya Mwanza na Yanga ya Dar es Salaam amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kiharusi.  
    Chama ni jina la utani ambalo marehemu Athumani Juma alipewa kutokana na beki wa zamani wa kimataifa wa Zambia, Dick Chama ambaye naye ni marehemu aliyecheza kwa mafanikio timu ya taifa ya kwao kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 1967 hadi 1976 na klabu za za Mufulira Wanderers, Green Buffaloes na Bancroft Blades.
    Athumani alipewa jina hilo baada ya kujiunga na Yanga SC mwaka 1981 akitokea Pamba ya Mwanza na mashabiki wa timu hiyo ya Jangwani walimbatiza Juma jina hilo baada ya beki wao mwingine, Rashid Idd aliyekuwa akiitwa Chama pia kuhamia Pan Africans baada ya kudumu Jangwani tangu 1979.
    Athumani Juma Chama (kulia) akisalimiwa na mchezaji mwenzake waliyecheza naye Yanga, Charles Boniface Mkwasa wiki mbili zilizopita aliupomtembelea hospitali 
    Na umaarufu wake zaidi Jangwani ukaja kutokana  na alivyoweza kumdhibiti mshambuliaji hatari wa mahasimu enzi hizo, Simba SC, Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’.
    Kisoka, Chama aliibukia Pamba FC ya Mwanza alikozaliwa na kukulia kabla ya kujiunga na Yanga SC na aliocheza nao wakati huo ni akina Joseph Fungo, Yussuf Ismail Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Isihaka Hassan Chukwu, Juma Mukambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba ‘JJ Masiga’, Elisha John, Ali Mchumila, Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omar Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengineo.
    Chama pia alikuwa akijulikana kwa jina lingine la utani, Jogoo ambalo alipewa mwaka 1981 kwenye michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya kutokana na mchezaji mmoja wa Harambee Stars, Sammy Onyango ‘Jogoo’. 
    Chama alistaafu soka mwaka 1990 na kujikita kwenye biashara zake ndogo ndogo kabla ya kuanza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2014 na kujikuta anashindwa kufanya shughuli yake hadi umauti wake.
    Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Chama. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ATHUMANI JUMA ‘CHAMA JOGOO’ AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top