TIMU ya Brazil imefanikiwa kufuzu Hatua ya 32 Bora Fanali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Scotland usiku wa jana wa Uwanja wa Hard Rock, Miami Gardens, Florida, Marekani.
Mabao ya Brazil yalifungwa na mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius José Paixão de Oliveira Júnior, mawili dakika ya saba na 45’+3, huku bao lingine likifungwa na kiungo wa Manchester United, Matheus Santos Carneiro da Cunha dakika ya 60.
Mchezo mwingine wa kundi hilo, Morocco nayo ilifanikiwa kwenda Hatua ya 32 Bora baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Haiti usiku wa jana Uwanja wa Mercedes-Benz mjini Atlanta, Georgia, Marekani.
Mabao ya Morocco yalifungwa na beki wa Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Achraf Hakimi Mouh dakika ya 39, mshambuliaji wa PSV Eindhoven ya Uholanzi, Ismael Saibari dakika ya 45’+1, wote wazaliwa wa Hispania, mshambuliaji wa Al Ain ya Falme za Kiarabu (UAE), Soufiane Rahimi dakika ya 78 na winga Gessime Ben Youssef Mustapha Yassine wa Strasbourg ya Ufaransa alikozaliwa dakika ya 89.
Mabao ya Haiti la kwanza alijifunga kipa wa Al Hilal ya Saudi Arabia, Yassine Bounou mzaliwa wa Canada dakika ya 10 na la pili akafunga mshambuliaji wa Sunderland ya England, Wilson Isidor mzaliwa wa Ufaransa dakika ya 43.
Msimamo wa Kundi C sasa ni Brazil kileleni kwa pointi zake saba, ikiizidi wastani wa mabao tu Morocco na zote zinafuzu Hatua ya Mtoano, wakati Scotland yenye pointi tatu na Haiti iliyomaliza bila pointi zinaaga mashindano.



.png)
0 comments:
Post a Comment