TIMU ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefanikiwa kutinga Hatua ya 32 Bora Fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Uzbekistan Alfajiri ya leo Uwanja wa Mercedes-Benz Jijini Atlanta, Georgia, Marekani.
Mabao ya DRC yamefungwa na washambuliaji, Yoane Wissa mzaliwa wa Ufaransa anayechezea klabu ya Newcastle United ya England dakika ya 68 kwa penalti na 90’+1 na Fiston Kalala Mayele wa Pyramids FC ya Misri dakika ya 78, huku bao pekee la Uzbekistan likifungwa na mshambuliaji pia, Eldor Azamat oʻgʻli Shomurodov wa İstanbul Başakşehir ya Uturuki dakika ya 10.
Mayele aliyewahi kuchezea klabu ya Yanga kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 anakuwa mchezaji wa kwanza kucheza timu ya Tanzania na Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwanza kucheza Fainali za Dunia na pili kufunga bao.
Huo ni mwendelezo wa rekodi nzuri za wachezaji waliowahi kucheza Yanga SC katika medani ya Kimataifa – kwani, Mkongo mwingine, Shabani Christophe Nonda ‘Papi’ baada ya kuwatumikia wana Jangwani mwaka 1994, alikwenda kuweka rekodi kadhaa Ulaya.
Rekodi hizo mchezaji wa kwanza kucheza Tanzania kucheza Ligi Kuu za Uswisi, Ufaransa, Italia na England na kuwa mchezaji wa kwanza na pekee hadi sasa kuwahi kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2003-2004 akiwa na AS Monaco ya Ufaransa ambayo ilifungwa 3-0 FC Porto ya Ureno iliyokuwa chini ya kocha Jose Mourinho.
Awali, kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Sunday Ramadhan Manara aliyecheza Yanga kuanzia mwaka 1971 hadi 1975 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ulaya aliposajiliwa na Heracles Almelo ya Ligi Kuu ya Uholanzi mwaka 1977.
Akaweka pia rekodi za kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ligi Kuu ya Marekani katika klabu ya New York Eagles kabla ya kwenda Austria kuchezea FC St. Veit na Falme za Kiarabu (UAE) kuchezea Al Nasr – kote huko Manara alifungua milango kama Mtanzania wa kwanza kufika na kucheza.
Mchezo mwingine wa mwisho wa kundi hilo, Colombia ililazimishwa sare ya bila mabao na Ureno Uwanja wa Hard Rock, Miami Gardens, Florida, Marekani.
Msimamo wa Kundi K sasa Colombia imeongoza kwa pointi zake saba ikifuatiwa na Ureno pointi tano na DRC pointi nne n azote zinakwenda Hatua ya 32 Bora, wakati Uzbekistan iliyopoteza mechi zote imeaga michuano.



.png)
0 comments:
Post a Comment