TIMU ya Singida Black Stars imeibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji Fc katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Airtel Mwigulu mjini Singida.
Ilikuwa ni siku nzuri kwa winga wa Mrundi, Mossi Nduwumwe aliyefunga hat-trick kwa mabao yake ya dakika za 27, 35 na 84, huku mabao mengine yakifungwa na kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Linda Mtange dakika ya 40 na mshambuliaji Mishamo Daudi Michael dakika ya 68.
Kwa ushindi huo, Singida Black Stars inafikisha pointi 47, ingawa inabaki nafasi ya nne nyuma ya Azam FC yenye pointi 58 baada ya timu zote kucheza mechi 27, wakati Dodoma Jiji FC inabaki na pointi zake 33 za mecgi 27 pia nafasi ya nane kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment