TIMU ya Uholanzi imefanikiwa kwenda Hatua ya 32 Bora Fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa Kundi F usiku wa jana Uwanja wa Arrowhead Jijini Kansas City, Missouri, Marekani.
Mabao ya Uholanzi yalifungwa na kiungo wa ulinzi wa Eintracht Frankfurt ya Ujerumani, Ellyes Joris Skhiri mzaliwa wa Ufaransa aliyejifunga dakika ya tatu, mshambuliaji Brian Ebenezer Adjei Brobbey wa Sunderland mwenye asili ya Ghana dakika ya saba na beki wa kati, Jan Paul van Hecke wa Tottenham Hotspur ya England dakika ya 62, huku bao pekee la Tunisia likifungwa na mshambuliaji wa Dynamo Makhachkala ya Uturuki, Hazem Mastouri dakika ya 54.
Mchezo mwingine wa Kundi F jana Japan ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Sweden Uwanja wa AT&T Jijini Arlington, Tarrant County, Texas, Marekani.
Mshambuliaji wa Celtic ya Scotland, Daizen Maeda alianza kuifungia Japan dakika ya 56, kabla ya mshambuliaji wa Newcastle United, Anthony David Junior Elanga kuisawazishia Sweden dakika ya 62.
Matoke ohayo yanamaanisha Uholanzi inamaliza kileleni mwa Kundi F kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Japan yenye pointi tano na Sweden pointi nne na zote zinafuzu Hatua ya 32 Bora – huku Tunisia iliyopteza mechi zote inaaga michuano.



.png)
0 comments:
Post a Comment