TIMU Coastal Union imeibuka na ushindi na I wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Wana Mangush yamefungwa na mshambuliaji Robert Pius Salula dakika ya tatu, kiungo Greyson Gerrard Gwalala ‘Tripple G’ dakika ya saba na mshambuliaji Thomas Emanuel Ulimwengu dakika ya 88, wakati bao pekee la KMC limefungwa na beki wa kati, Mudathir Nassor dakika ya 30 kwa penalti.
Kwa ushindi huo, Coastal Union inafikisha pointi 32 katika mchezo wa 27 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tisa, ikiishushia nafasi ya 10 Fountain Gate FC yenye pointi 29 za mechi 26.
Kwa upande wao KMC ambao tayari wamekwishashuka daraja — baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao tisa wakiendelea kushika mkia kwenye ligi ya timu 16 kufuatia kucheza mechi 27.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment