WENYEJI, Tanzania Prisons wameibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Francisco Lulihoshi kwa penalti dakika ya pili, Oscar Mwajanga dakika ya 12 na Jeremiah Juma dakika ya 66, wakati bao pekee la Dodoma Jiji FC limefungwa na Waziri Junior dakika ya 43.
Kwa ushindi huo, Tanzania Prisons inafikisha pointi 23, ingawa inabaki nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16 mbele ya KMC FC inayoshika mkia kwa pointi zake tisa baada ya timu hizo zote kucheza mechi 26.
Kwa upande wao Dodoma Jiji FC pamoja na kupoteza mchezo huo wanabaki nafasi ya nane wakiwa na pointi 33 wakizidiwa tu wastani wa mabao na Pamba Jiji FC baada ya timu hizo kuchea mechi 26.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment