• HABARI MPYA

  Wednesday, May 03, 2023

  HONGERA YANGA, TUNATARAJIA KOMBE LA KWANZA LA AFRIKA TANZANIA


  MABINGWA wa Tanzania, hatimaye wameweka historia ya kufika Nusu Fainali ya michuano ya klabu Afrika baada ya kuitoa Rivers United ya Nigeria kufuatia sare ya 0-0 katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Jumapili Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Yanga imekwenda Nusu Fainali kwa faida ya ushindi wa 2-0 ugenini kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyotangulia nchini Nigeria, mabao ya mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele kipindi cha pili.
  Yanga sasa itamenyana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo imeitoa Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Cairo kwenye mechi ya kwanza na kushinda 1-0 mchezo wa marudiano Phokeng, NW Jumapili.
  Mechi ya kwanza Yanga na Marumo Gallants itafanyika Dar es Salaam Mei 10 na marudiano yatafuatia Afrika Kusini Mei 17.
  Ni mara ya kwanza kabisa kwa Yanga kwenda Nusu Fainali ya michuano yoyote ya Afrika baada ya kukomea Robo Fainali mara nne awali, mara tatu katika Ligi ya Mabingwa 1969, 1970 na 1998 na mara moja katika Kombe la Washindi 1995. 
  Mwaka 1974 Simba iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika Nusu Fainali ya Michuano ya Afrika, ilikuwa klabu bingwa Afrika ilipoitoa Hearts Of Oak ya Ghana kwa ushindi wa 2-1 Accrah mabao ya Adamu Sabu (marehemu) na Abdallah Kibadeni na sare ya 0-0 Dar es Salaam.
  Simba ikaenda kutolewa Ghazl El Mahalla ya Misri kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0, bao la Wekundu wa Msimbazi hapa Dar es Salaam likifungwa na Saad Ally.
  Mwaka 1993 Simba ikaandika historia ambayo bado haijavunjwa, kufika Fainali ya Kombe la CAF kufuatia kuwatoa  Atlético Sport Aviação (ASA) kwa mabao 3-1 Dar es Salaam na sare ya 0-0 Jijini Luanda, Angola – na kwenye Fainali ikafungwa 2-0 na Stella Adjamé ya Ivory Coast hapa hapa Dar es Salaam ikitoka kutoa sare ya 0-0 Abidjan.
  Mwaka 1995 Malindi ya Zanzibar nayo ikafika Nusu Fainali ya Kombe la CAF kufuatia kuitoa OC Agaza ya Togo kwa ushindi wa 2-0 ugenini pia kufuatia sare ya 0-0 Zanzibar na yenyewe ikaenda kutolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 kwake.
  Mwaka 2003 Simba wakafika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 kwake.
  Kama ilivyokuwa mwaka 1998, Robo Fainali za 2003 pia zilichezwa kwa mtindo wa makundi ambao sasa umebadilishwa makundi ni 16 Bora.
  Yanga sasa wanakwenda kuwania kuvunja rekodi ya Simba ya kuwa timu pekee ya Tanzania kufika Fainali ya michuano ya klabu barani Afrika katika mechi mbili kali dhidi ya mpinzani mgumu kutoka Afrika Kusini.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Yanga kwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kusema imeandika historia Jalili.
  “Pongezi kwa Klabu ya Yanga kwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup), na kila la kheri katika maandalizi mliyoanza sasa kwa mchezo ujao. Mmeandika historia jalili,”amesema Rais Samia na kuongoza;
  “Mmetuheshimisha sana. Hamasa yangu inaendelea, na sasa imeongezeka. Kaifanyeni kazi,”.
  Ni kweli, Yanga wameiheshimisha Tanzania kwa mafanikio yao hayo katika kipindi ambacho klabu nyingine kubwa ya Tanzania, Simba SC imekuwa ikikomea hatua ya Robo Fainali mfululizo, iwe Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho.
  Yanga wanahitaji kujipanga vyema kwa mechi hizo mbili dhidi ya Marumo Gallants, kwani nayo inaonekana ni timu ambayo ipo ndani ya uwezo wao na kama wataingia kwa maarifa yale yale yaliyowafikisha hapa – hapana shaka Fainali inawahusu.   
  Hongera Yanga kwa mafaniko yenu chini ya kocha mtaalamu kabisa Nasredine Mohamed Nabi raia wa Tunisia, na kama alivyosema Mheshimiwa Rais Dk. Samia, mmeiheshimisha nchi. Kila la heri katika hatua zijazo, tunatarajia Kombe la kwanza la Afrika hapa Tanzania mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HONGERA YANGA, TUNATARAJIA KOMBE LA KWANZA LA AFRIKA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top