• HABARI MPYA

    Tuesday, February 11, 2020

    MORRISON AINUSURU YANGA SC KUCHAPWA NA MBEYA CITY TAIFA, YAAMBULIA SARE YA 1-1

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VIGOGO, Yanga SC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
    Sare hiyo inazidi kuwatoa Yanga SC kwenye mbio za ubingwa, kwani wakifikisha pointi 38 katika mchezo wa 19 wanazidiwa pointi sita na Azam FC na pointi 15 na mabingwa watetezi, Simba SC.
    Katika mchezo wa leo, Mbeya City waliitangulia Yanga SC kwa bao la kujifunga la beki Mghana, Lamine Moro aliyekuwa anajaribu kuutoa nje mpira uliopigwa na Rehani Kibingu dakika ya 41.



    Kutoka hapo, Mbeya City inayofundishwa na beki wa zamani wa Simba SC, Amri Said ‘Stam’ ikaanza kucheza kwa kujilinda zaidi kuwazuia Yanga kupata bao.
    Lakini pia wachezaji wa safu ya ushambuliaji ya Yanga SC nao hawakuwa na bahati, kwani walipoteza nafasi nyingi za wazi walizotengenezewa.
    Hatimaye kiungo Mghana, Bernard Morison akaifungia Yanga SC bao la kusawazisha dakika ya 75 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia, Juma Abdul.
    Mbeya City waliendelea kucheza kwa kujihami – huku Yanga wakiendelea kupoteza nafasi zaidi za kufunga hata baada ya kuingia kwa Tarek Seif na Deus Kaseke kuchukua nafasi za David Molinga na Ditram Nchimbi.
    Mbeya City imefanikiwa kutofungwa na Yanga msimu huu, baada ya kutoka sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Desemba 24, mwaka jana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.  
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Lamine Moro, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Papy Kabamba Tshishimbi, Ditram Nchimbi/ Deus Kaseke dk77, Haruna Niyonzima, David Molinga/Tariq Seif dk63, Balama Mapinduzi na Bernard Morrison.
    Mbeya City; Haroun Mandanda, Kenneth Kunambi/ Samson Madeleka dk73, Hassan Mwasapili, Ibrahim Ndunguli, Roland Msonjo, Emmanuel Memba, Rehani Kibingu, Ally Nassor/George Chota dk81, Abasarim Chidiebele, Peter Mapunda/Mohammed Mussa dk86 na Suleiman Ibrahim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MORRISON AINUSURU YANGA SC KUCHAPWA NA MBEYA CITY TAIFA, YAAMBULIA SARE YA 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top