• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 01, 2020

  ‘BI DADA’ JEONESIA RUKYAA KUCHEZESHA TENA MECHI YA WATANI, SIMBA NA YANGA JUMAMOSI TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  REFA wa kike, Jeonesia Rukyaa atachezesha mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga itakayofanyika Jumamosi kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
  Jeonesia mwenye uzoefu sasa wa kuchezesha mechi hizo, Jumamosi atasaidiwa na washika vibendera Soud Lila na Hamisi Chang’walu wote wa Dar es Salaam.
  Refa wa akiba atakuwa Heri Sasii wa Dar es Salaam, Kamishna Khalid Bitebo ‘Zembwela’ kutoka Mwanza na Mtathmini Mchezo, Soud Abdi wa Arusha.

  Katika mechi mbili za msimu uliopita baina ya wababe hao wa soka ya Tanzania, ya kwanza ilimalizika kwa sare ya 0-0 Septemba 30, mwaka 2018 na ya pili Simba SC ikashinda 1-0 bao pekee la Meddie Kagere dakika ya 72 Februari 16, mwaka 2019 msimu ambao Wekundu wa Msimbazi waliibuka tena mabingwa wa Ligi Kuu.
  Ni msimu ambao Simba SC ilikuwa chini ya kocha Mbelgiji Patrick J. Aussems na Yanga walikuwa na Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao wote wamefukuzwa wakifuatana Novemba na Desemba.
  Nafasi ya Aussems imechukuliwa na Mbelgiji mwenzake, Sven Ludwig Vandenbroeck wakati Yanga kwa sasa ipo chini ya gwiji wake, Charles Boniface Mkwasa.
  Simba SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 34 baada ya kucheza mechi 13, ikiwazidi pointi 10 mahasimu wao hao wa jadi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘BI DADA’ JEONESIA RUKYAA KUCHEZESHA TENA MECHI YA WATANI, SIMBA NA YANGA JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top