• HABARI MPYA

  Sunday, October 06, 2019

  YANGA SC WAFUTA ‘MKOSI’ LIGI KUU YA TANZANIA BARA, YAITANDIKA COASTAL UNION 1-0 DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imepata ushindi wake wa kwanza katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Coastal Union 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee leo, kiungo Abdulaziz Makame ‘Bui’ dakika ya 51 akimalizia kwa kichwa pasi ya kichwa beki Ali Hamad Ali kufuatia kona ya kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa.
  Hata hivyo, wachezaji wa Coastal Union walimlalamikia refa Abubabar Mturo wa Mtwara wakidai mpira uliokolewa kabla ya kuvuka mstari wa goli. 
  Hata hivyo, utata ulisababishwa na msaidizi namba mbili wa refa, Credo Mbuya aliyenyoosha kibendera kuashiria wachezaji wa Yanga wameotea, wakati kulikuwa kuna mlinzi wa Coastal Union ndani ya lango.  Ikicheza kwa mara ya pili mfululizo bila kocha wake Mkuu, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) anayetumikia adhabu ya kufungiwa na Bodi ya Ligi, Yanga SC leo kidogo ilijitahidi kumiliki mpira na kutengeneza nafasi zaidi, japo walitumia hiyo moja tu.
  Mshambuliaji Mkongo, David Molinga ‘Falcao’ aliyefunga mabao mawili katika sare ya 3-3 na Polisi Tanzania kwenye mchezo uliopita leo hakuwa na bahati sawa na Ngassa kutokana na wote kukosa mabao ya wazi. 
  Ikumbukwe mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Yanga SC ilichapwa 1-0 na Ruvu Shooting hapo hapo Uwanja wa Uhuru na tangu hapo haikushinda tena hadi leo, ikitoa sare ya 1-1 na kufungwa 2-1 na Zesco United katika Ligi ya Mabingwa, kabla ya sare nyingine ya 3-3 na Polisi.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikalo, Juma Abdul, Ally Mtoni ‘Sonso’, Ali Hamad, Kelvin Yondan/Mustafa Suleiman dk80, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Abdulaziz Makame, David Molinga, Mapinduzi Balama na Deus Kaseke/Jafary Mohamed dk71.
  Coastal Union; Soud Abdallah, Hassan Kibailo, Omary Salum, Stanley Kennedy, Bakari Nondo, Mtenje Albano, Hajji Ugando/Hamisi Kanduru dk57, Ayoub Semtawa, Shaaban Iddi, Menzi Chili/Prosper Mushi dk64  na Ayoub Lyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WAFUTA ‘MKOSI’ LIGI KUU YA TANZANIA BARA, YAITANDIKA COASTAL UNION 1-0 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top