• HABARI MPYA

    Wednesday, February 13, 2019

    HANS MABENA KUCHEZESHA MECHI YA WATANI, SIMBA NA YANGA JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa mahasimu wa jadi, Yanga SC na Simba SC utakaofanyika Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam utachezeshwa na refa Hans Mabena kutoka Tanga.
    Bodi ya Ligi Tanzania (TLB) imetaja marafa watakaotumika kwenye mechi hiyo na Mabena atasaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono na Kassim Mpanga, wakati Heri Sasi atakuwa refa wa akiba.
    Watani wa jadi, Simba na Yanga wanakutana Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baada ya timu hizo kutoka sare ya 0-0 kwenye mechi ya kwanza Septemba 30, mwaka jana Uwanja wa Taifa.

    Hans Mabena (katikati) atachezesha mechi ya watani wa jadi Jumamosi Uwanja wa Taifa

    Mchezo wa Jumamosi unakuja wakati Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 58 za mechi 23, ikiizidi pointi tisa Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili, ingawa ina mechi mbili mkononi, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 36 za mechi 15.
    Viingilio katika mchezo wa Jumamosi vinatarajiwa kuwa Sh. 7,000 kwa mzunguko, Sh. 20,000 VIP B na C na Sh. 30,000 kwa VIP A.
    Simba SC imeweka kambi katika hoteli ya Sea Scape eneo la Kunduchi, Dar es Salaam ikifanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, wakati Yanga SC ipo mjini Morogoro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS MABENA KUCHEZESHA MECHI YA WATANI, SIMBA NA YANGA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top