• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 25, 2019

  HIMID MAO AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO PETROJET IKISHINDA 2-0 UGENINI MISRI

  Na Mwandishi Wetu, CAIRO
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Himid Mao Mkami leo amefunga bao lake la kwanza kabisa katika klabu ya Petrojet ikiibuka na ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya El Daklyeh katika mchezo wa Ligi Kuu ya Misri Uwanja wa Al-Shorta mjini Cairo.
  Himid, mchezaji wa zamani wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, alifunga bao hilo dakika ya tano ya muda wa ziada baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo huo.
  Na Himid aliyekuwa anacheza mechi yake ya 19 tangu asajiliwe Petrojet Juni mwaka jana kutoka Azam FC alifunga bao hilo baada ya mshambuliaji Mmisri, Shokry Naguib kufunga la kwanza dakika ya 42. 

  Himid Mao leo amefunga bao lake la kwanza Petrojet ikishinda 2-0 dhidi ya El Daklyeh

  Kwa ushindi huo, Petrojet inafikisha pointi 25 katika mechi ya 24 ikijiinua kutoka nafasi ya 14 hadi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Misri inayoshirikisha timu 18.
  Hali ni mbaya kwa ENPPI anayochezea kwa mkopo kiungo mshambuliaji Mtanzania, Shiza Kichuya kwa mkopo kutoka Pharco ya Daraja la Pili, ikiwa inashika nafasi ya 17 kwa pointi zake 21 za mechi 22. 
  Ismailia, timu nyingine yenye mchezaji Mtanzania, mshambuliaji Yahya Zayd yenyewe inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 27 za mechi 19. Kichuya, mchezaji wa zamani wa Simba na Zayd kutoka Azam FC wote wamejiunga na klabu za Misri Januari mwaka huu.
  Himid Mao (kulia) akiwa na Shiza Kichuya (kushoto) baada ya kukutana mjini Cairo mwishoni mwa wiki
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HIMID MAO AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO PETROJET IKISHINDA 2-0 UGENINI MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top