• HABARI MPYA

    Wednesday, February 27, 2019

    ALLIANCE WAHAMISHIE MAFANIKIO YAO YA DARASANI KATIKA SOKA

    Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
    NI matumaini yangu kwamba mnaendelea vizuri na shughuli za hapa na pale hasa za kimichezo na masomo. Kama mnavyoona hapo juu, barua yangu ina kichwa lakini haina anuani ya mwandikiwa. Hii ni ishara kwamba ni barua ya kirafiki kutoka kwangu kuja kwenu. Nina mambo machache nataka kuwapongeza na panapobidi niwape ushauri wangu mdogo katika mbio zenu za kufikia vilele vya mafanikio. Kwa kuwa hii ni barua ya kirafiki, haifungwi na urefu hivyo naomba muisome yote bila kuishia njiani.
    Mimi ni miongoni mwa vijana waliovutiwa sana na mfumo wa uendeshaji wa academi yenu ya michezo. Kilichonivutia zaidi ni kuona vijana wadogo, wanafunzi wakifanya vizuri sana kwenye kila mashindano ya ndani na nje ya nchi mlioshiriki.
    Sijui kwanini nilikuwa na mahaba na timu yenu. Labda ni kwa sababu na mimi kipindi hicho nilikuwa mwanafunzi wa Sekondari kama miongoni mwa wachezaji wenu.
    Nilifurahi zaidi nilipoona nia yenu ya kutaka kushiriki ligi kuu Tanzania (wakati huo ikiitwa VPL).  Nami nikaazimia moyoni kwamba, nitakuwa shabiki wa Alliance kama watapanda ligi kuu. 
    Mpira wenu wa kuvutia wenye kila udambwi dambwi uliochagizwa na uwezo wa vijana wanyumbulifu wenye vipaji lukuki, uliwafanya mpigiwe shangwe na nderemo kila mlipocheza.
    Nakumbuka kuna mechi moja mlicheza huko kwetu Rorya, pale Shirati dhidi ya Rorya Combine na kuwalaza watu wazima hao mabao 3-0. Watu wakasema, hawa watoto wameiva. Nawakumbusha tu, sijui mnakumbuka hili au mmeshasahau?
    Msimu wa mwaka 2016/2017 mkiwa na kikosi bora kabisa kwenye ligi daraja la kwanza, niliamini kwamba mnapanda ligi kuu. Lakini kichapo cha mabao 2-0 mlichopata pale Namfua katika mechi yenu ya mwisho dhidi ya Singida united kiliwanyima fursa. Msimu huo, Singida iliyokuwa chini ya Fred Felix Minziro ilipanda ligi kuu huku nyie mkibaki ligi daraja la kwanza. Wakazi wa Mwanza na watu wenye mahaba nanyi waliumia sana lakini, mkasema ngoja mjipange msimu ujao.
    Msimu uliofuatia, mwaka 2017/2018 ndipo kwa mara ya kwanza Alliance ikapata tiketi ya  kupanda ligi kuu. Lakini safari haikuwa nyepesi kwani iliwalazimu kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Biashara united ya Mara ambayo ilikuwa vizuri sana mwaka ule. Ndipo Biashara na Alliance zikapanda ligi kuu kutoka kundi C.
    Sijui ni ugeni wa ligi, sijui kulikuwa na tatizo gani ila ninachokijua ni kwamba mlianza ligi vibaya sana katika msimu wenu wa kwanza kwenye ligi kuu Tanzania (TPL) mwaka 2018/2019. Watanzania wakaanza kuwatabiria mapema kwamba mtarudi mlikotoka.
    Mkurugenzi wa Alliance, ndugu James Marwa Bwire, mtu asiyetaka kushindwa hakufurahishwa na hali ile. Ndipo akaanza kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi. Ikambidi Mbwana Makata ampishe Baptiste Kayiranga.
    Mambo yakawa bado hayaeleweki. Ndipo Malale Hamsini akapewa jukumu la kuinoa Alliance kama kocha mkuu na kusaini mkataba wenye makubaliano ya kuibakisha timu kwenye nafasi 10 za juu mwishino mwa msimu.
    Sasa mko nafasi ya 7 na alama zenu 36 sawa na ndugu zenu Mbao FC lakini wako juu yenu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. 
    Sijui kama mnafuatilia hali ya majirani zenu kutoka Musoma, Biashara united. Kama hamjui, niwape taarifa tu kwamba hali yao si nzuri. Licha ya kuwa juu yenu wakati wa kupanda ligi kuu, sasa hivi wanahangaika kujinasua kutoka kwenye msatri mwekundu wa kushuka daraja. Nawagusia tu maana huu ndio ujirani mwema. Urefu wa kutoka kwenu Ilemela mpaka kwao Musoma ni sawa na ule wa pua na mdomo.
    Wachezaji wenu wamezidi kuonesha ukomavu zaidi kwenye ligi. Kitendo cha Dickson Ambundo kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari huku akiwa miongoni mwa wanaoongoza kwa kufumania nyavu, hudhihirisha kwamba Alliance imekuwa.
    Sitaki barua yangu iwachoshe kabla sijawaambia lengo langu kubwa la kuamua kutumia vidole vyangu kubofya vibonyezeo vya simu yangu janja kufikisha ujumbe huu kwenu.
    Hongereni kwa kuwa miongoni mwa timu zilizoingia kwenye hatua ya 8 bora ya kombe la shirikisho la TFF (ASFC). Bingwa wa kombe hili ndiye huiwakilisha nchi kimataifa katika kombe la shirikisho la CAF.
    Kwa hali hiyo, nichukue fursa hii kuwashauri mtumie nguvu nyingi sana huku kuliko hata kwenye ligi kuu. Mko kwenye robo fainali sasa. Mkishinda mechi tatu zilizobaki, mnachukua ubingwa.
    Hili ni jambo la msingi zaidi. Najua hamwezi kuchukua ubingwa wa TPL wala kushuka daraja lakini mnaweza kuchukua ASFC. Kwenye ligi mmebakisha mechi 10 ambazo hata mkishinda zote, hamchukui ubingwa. Lakini hapa mkishinda mechi 3 zilizobaki, mwakani mnapanda ndege kwenda Alexandria, Johannesburg, Ouagadougou na kwingineko barani Afrika.
    Au mnaogopa kuchukua ubingwa kisa mtakutana na akina Wydad Casablanca, El Hilal  na Asante Kotoko? Hapana. Sidhani kama mnaogopa. Hamjawahi wala hamna mpango wa kuogopa mechi kubwa.
    Ni shauku ya Watanzania kuona timu mpya zikishiriki michuano ya kimataifa kama walivyofanya Mtibwa mwaka jana.
    Wapo watakaowabeza kwamba nyie ni timu ndogo, lakini wakiwaambia hivyo, muwakumbushe kwa kuwauliza swali la tashtiti kwamba je, ni mara ngapi timu za Kariakoo mnazoziita "timu kubwa" zimeshiriki michuano hii bila mafanikio? Msitake majibu kutoka kwao. Msibishane nao mitandaoni bali dakika 90 zitoe majibu ya kuwatahayarisha.
    Kama ambavyo shule zenu pale Mahina Mwanza zinavyopambana kuingia kwenye shule 10 bora kitaifa, vivyo hivyo na nyie mpambane kushiriki soka la kimataifa. Pesa mnazo, uwezo mnao na kila sababu ya kuwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika. Amueni sasa kufanya hivyo. Kila la heri Alliance  Schools Football Club.
    (Frederick Daudi ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC). Anapatikana kwa namba 0742164329 na e-mail defederico131@gmail.com).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALLIANCE WAHAMISHIE MAFANIKIO YAO YA DARASANI KATIKA SOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top