• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 22, 2019

  SAMATTA ATUPWA NJE EUROPA LEAGUE BAADA YA GENK KUTANDIKWA 4-1 UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  SAFARI ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kwenye michuano ya Europa League imefikia tamati katika hatua ya 32 Bora baada ya klabu yake, KRC Genk kutolewa kufuatia kipigo cha mabao 4-1 nyumbani, Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk mbele ya SK Slavia Praha ya Jamhuri ya Czech.
  Ni kipigo cha kushitua, kwani Genk ilipewa nafasi kubwa ya kwenda hatua ya 16 Bora baada ya kulazimisha sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza huko Czech Siku ya Wapendano.
  Na hata jana Genk iliuanza vizuri mchezo ikitangulia kwa bao la Leandro Trossard dakika ya 10, kabla ya Slavia Praha kugeuza kibao na kuwanyamazisha wenyeji.

  Kipa Ondrej Kolar wa Slavia Praha akidaka dhidi ya mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta jana

  Mabao ya Slavia Praha yalifungwa na Vladimir Coufal dakika ya 23, Ibrahim Traore dakika ya 53 na Milan Skoda mawili dakika za 64 na 68 katika usiku ambao Samatta aliwekwa chini ya ulinzi mkali na kukosa nafasi ya kufunga.
  Genk ilipata pigo baada ya kipa wao wa kwanza, Muaustralia, Danny Vukovic kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na kinda Mbelgiji, Nordin Jackers mwenye umri wa miaka 21 aliyekwenda kuruhusu mabao mawili ya Skoda.  
  Samatta mwenye umri wa miaka 26, jana amecheza mechi ya 24 ya Europa League, akiwa amefunga mabao 14 – inayomfanya awe amecheza jumla ya mechi 144 za mashindano yote na kufunga mabao 59 tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Mbwana Samatta akiwa katikati ya mabeki wa Slavia Praha jana Uwanja wa Luminus Arena 

  Safari ya Genk kwenye michuano ya Europa League msimu huu imefikia tamati jana

  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 111 na kufunga mabao 44 na kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic/Jackers dk59, Maehle, Dewaest, Lucumi, De Norre/Uronen dk56, Heynen/Wouters dk29, Malinovsky, Pozuelo, Ito, Trossard na Samatta.
  Slavia Prague; Kolar, Coufal, Zmrhal, Kudela, Bofil, Deli, Skoda, Soucek, Traore/Stoch dk64, Masopust/Olayinka dk66 na Kral.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ATUPWA NJE EUROPA LEAGUE BAADA YA GENK KUTANDIKWA 4-1 UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top