• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 27, 2019

  JAPOKUWA AZAM FC NA YANGA ZINAPEWA NAFASI KUBWA ASFC, LAKINI…

  Na Frederick Daud, DAR ES SALAAM
  KAMA kuna kitu ambacho Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanya vizuri, ni kutoa nafasi ya bingwa wa kombe la shirikisho hilo (ASFC) kushiriki michuano ya kimataifa.
  Wasingefanya hivyo, pengine michuano hii ingekosa mvuto kwani timu zisingetilia maanani bali wangekuwa wanachezesha vikosi dhaifu ili kutunza vikosi vyao kwa ajili ya ligi kuu.
  ASFC inatoa fursa kwa timu yoyote inayoibuka na ubingwa kucheza Kombe la shirikisho barani Afrika. Hii haijalishi uko daraja la pili, daraja la kwanza au ligi kuu. Yaani kuna uwezekano wa kuzikutanisha Nyarugusu ya Geita au Mashujaa ya kigoma na TP Mazembe ya DRC au Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
  Mwaka huu tayari michuano hii imefika kwenye hatua ya Robo fainali ambapo African Lyon, Alliance, Azam, Kagera Sugar, KMC, Lipuli, Singida United na Yanga zimefanikiwa kufuzu. Kongole kwa timu hizi nane bora.
  Ningepata fursa ya kuishauri timu mojawapo kati ya hizi nane ambazo zote zinacheza ligi kuu, ningewaambia watumie nguvu nyingi huku kuliko kwenye ligi kuu.
  Ndio, wanapaswa kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu katika hatua hii waliyofikia, ukishinda mechi tatu zilizobaki (robo fainali, nusu fainali na fainali), unachukua ubingwa. Si hilo, tu bali unapata fursa ya kupanda ndege kushiriki michuano ya CAF.
  Tofauti na ligi kuu ambapo bado mechi nyingi sana. Halafu uhakika wa kuchukua ubingwa wa ligi ni mdogo sana kwa baadhi ya timu. Kiujumla, ukiachana na Yanga na Azam, hakuna timu nyingine kati ya hizi nane yenye uelekeo wa kuchukua ubingwa wa TPL.
  Hapa ndipo unagundua kwamba Yanga na Azam zina nafasi kubwa zaidi maana wanaweza kuchukua ubingwa wa TPL au ASFC hivyo mwakani wakaiwakilisha nchi kimataifa. Hawa ndio vinara kwenye ligi lakini pia hata kwenye hatua hii ya robo fainali, wao ndio wanapewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa.
  Lakini je, wajua? Yanga na Azam bado zinaweza zikashindwa kuiwakilisha nchi kimataifa. Kuongoza ligi na kuingia nane bora ya ASFC hakuwapi garantii ya kucheza michuano ya CAF. Suala siyo kuongoza ligi, suala ni kuchukua ubingwa.
  Kwenye ligi kule kuna bingwa mtetezi, Simba ambaye baada ya kutolewa kwenye kombe hili la TFF, wameelekeza nguvu zao kwenye ligi kuu. Japo wako nafasi ya tatu lakini kasi yao na hari waliyonayo inaashiria jambo fulani. Kumbuka wameshaonja utamu wa kufika 16 bora ya klabu bingwa Afrika na hawataki wakosekane kwenye michuano hiyo mwakani. Hivyo lolote linaweza likatokea.
  Hata kwenye ASFC pia, usije ukashangaa kuwaona Azam na Yanga wakikosa ubingwa. Licha ya kwamba wao ni timu bora na kubwa kuliko zingine kwenye hatua hii, hawapaswi kubweteka. Suala la mshika mawili moja kumponyoka au kuponyokwa na yote mawili ni jambo la kawaida tu.
  Timu kama Singida united ambayo baada ya kufika fainali mwaka jana na kuukosa ubingwa, mwaka huu wana shauku kubwa ya kufanya vizuri zaidi ya mwaka jana. Hata hawa kina Lipuli na nyinginezo, ni timu za kuangalia kwa jicho la tatu au hata la nne kama lipo.
  Msimu uliopita Azam na Yanga wote hawakushiriki michuano ya kimataifa baada ya Simba kuchukua VPL ambayo sasa ni TPL na Mtibwa kuibuka na Ubingwa wa michuano hii ya TFF inayodhaminiwa na Azam. Huu ndio wakati wa Azam na Yanga kufanya hivyo, japo siyo kirahisirahisi tu maana hata Maandiko Matakatifu yamewataka wanaume kula kwa jasho. Lazima wapambane.
  Enyi Azam na Yanga, ni kweli ninyi ni vinara kwenye mbio za ubingwa wa TPL. Sina wasiwasi kwamba nyie ni timu bora ukilinganisha na sita zingine zilizoingia robo fainali. Hayo kila Mtanzania anayatambua. Tahadhari ni kwamba, uwezekano wa kukosa nafasi zote mbili upo pia. Chagueni wenyewe. Kama mnataka kusuka au kunyoa saluni zipo za kutosha tu hapa mjini. Mimi nimewatahadharisha mapema kabisa ili msije mkanilaumu hapo baadaye.
  (Frederick Daudi ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC). Anapatikana kwa namba 0742164329 na e-mail defederico131@gmail.com).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JAPOKUWA AZAM FC NA YANGA ZINAPEWA NAFASI KUBWA ASFC, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top